HIVI karibuni wanajeshi wa Korea Kaskazini walifanya gwaride maalum ambapo mgeni rasmi kwenye gwaride hilo lililofanyika mjini Pyongyang, alikuwa kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong-un
Madhumuni ya kufanyika kwa gwaride hilo, ilikuwa ni maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 75 ya chama cha wafanyakazi kinachotawala katika taifa hilo liliopo mashariki ya mbali.
Waandishi wakiwa nje ya nchi waliofuatilia hafla hiyo waliripoti kwamba sherehe hiyo iliambatana na maonesho ya makombora ya makubwa ambayo hayakuonekana yalioneshwa.
Hilo lilikuwa gwaride la kwanza na maonesho ya kwanza ya makombora nchini humo katika kipindi cha miaka miwili na inakuja wiki chache kabla ya uchaguzi wa urais wa Marekani.
Korea Kaskazini imejizuia kuonesha makombora ya masafa marefu katika gwaride tangu rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa taifa hilo Kim Jong-Un walipofanya mkutano wao wa kwanza mnamo 2018.
Kwa mujibu wa jeshi la Korea Kusini, gwaride hilo lilifanyika kabla ya alfajiri na sababu za kufanyika gwaride hilo muda huo bado hazijafahamika.
Aidha Korea Kusini ilisema kuwa kabla ya kufanyika kwa gawaride hilo, kiongozi wa taifa hilo Kim Jong-un aliitishwa mkutano wa dharura wa baraza la usalama la taifa kujadili suala la silaha za kuoneshwa sambamba na yaliyomo kwenye hotuba ya Kim Jong-un aliyopanga kuitoa.
Katika hafla hiyo ya Pyongyang hakuna vyombo vya habari vya kigeni au wageni waliruhusiwa kuhudhuria, kwa hivyo wachambuzi wanategemea picha zilizopigwa na vyombo vya habari vya ndani ambazo zinatolewa kutathmini gwaride hilo.
Miongoni mwa kombora lililooneshwa ni lile ambalo lilionekana kama la masafa marefu (ICBM) linaloweza kufika katika bara jingine ambalo ni kubwa kuliko kombora lolote la Korea Kaskazini.
Kwanza ilipitishwa kombora lililozinduliwa la nyambizi Pukguksong 4A, ikifuatiwa na kombora kubwa la Intercontinental Ballistic (ICBM) kwenye gari la kurushia na magari aina ya colossal ‘axles’ 11 mapya ambayo haijulikani yamepewa majina gani.
Kombora jengine lililoneshwa katika hafla hiyo ya miaka 75 ya chama cha wafanyakazi, linaonekana kama limefanyiwa mabadiliko ambalo linaweza kufyatuliwa kutoka katika nyambizi.
Wakati baadhi ya wataalamu wanasema inaweza kuwa ni makombora ya mfano tu ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi, kuoneshwa kwao hadharani kunaonesha kuwa Korea kaskazini inaendelea kusogea mbele katika kuimarisha uwezo wake wa silaha.
Wachambuzi waliofuatilia hafla hiyo iliyooneshwa mtandaoni wameona wanajeshi wakiwa na silaha mpya za mashambulizi, pamoja na kile kinachoonekana kama mifumo mpya ya ulinzi wa anga na gari za kivita.
Hata hivyo wanaeleza kuwa kusita kwa mazungumzo baina ya Marekani na taifa hilo, kunaongeza kasi kwa utawala wa Pyongyang kuendelea kutengeneza makombora.
Makombora
Picha hizo ilimuonesha kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong-un akiwa amevaa suti ya kijivu iliyoshonwa kwa mtindo wa magharibi, akipokea maua kutoka kwa watoto.
Katika hotuba, Kim alisema Korea Kaskazini itaendelea na jitihada zake za kujiimarisha kijeshi kwa lengo la kujilinda dhidi ya maadui wa taifa hilo.
Kiongozi huyo wa Korea kaskazini Kim Jong-un alionya kwamba atatumia uwezo wake wote wa kinyuklia iwapo atatishiwa lakini aliepuka kuikosoa moja Marekani.
Alisema pia anashukuru kwamba hakuna wakorea wa Kaskazini walio na maambukizi Covid-19. “Ninawatakia afya njema watu wote ulimwenguni ambao wanapambana na shida za virusi hivi viovu,” alisema.
Licha ya kudai kuwa nchi hiyo haina mgonjwa wa corona, Kim anaendelea kufanya mikutano ya kiwango cha juu kuhakikisha masharti ya kupambana na ugonjwa huo yanatekelezwa ipasavyo.
Wachambuzi wamesema haiwezekani kwamba Korea Kaskazini kuwa haijapata kesi za maambukizi ya virusi vya corona, hata hivyo inawezekana anachofanya kiongozi huyo ni propaganda. Hakukuwa na ishara ya mtu yeyote aliyevaa barakoa wakati wa gwaride.
Akizungumzia suala hilo, wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imesema ina wasi wasi juu ya ukweli kwamba Korea Kaskazini imeonesha silaha ikiwa ni pamoja na zile zilizokuwa zinashukiwa kuwa makombora mapya ya masafa marefu.
Taarifa ya wizara iliitaka Korea Kaskazini kuendelea kuwa sehemu ya makubaliano ya pamoja ya Korea ya mwaka 2018 yenye lengo la kupunguza uadui baina yao.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Korea Kusini imetoa taarifa tofauti inayoitaka Korea Kaskazini kurejea katika mazungumzo ili kupiga hatua katika nia yake thabiti ya kufikia kutokuwa na silaha za kinyuklia na amani katika rasi ya Korea.
Baada ya mkutano wa dharura wa baraza la usalama la taifa, wajumbe wa baraza hilo nchini Korea Kusini walisema wataendelea na kufanya tathmini mkakati wa mfumo wa silaha wa Korea Kaskazini uliooneshwa na kufanya mapitio mapya ya uwezo wa ulinzi wa Korea Kusini.
Mahusiano kati ya Korea mbili yanaendelea kuwa mabaya huku kukiwa na mkwamo wa diplomasia ya kinyuklia kati ya Pyongyang na Washington, hali inayoongeza wasi wasi katika eneo hilo.