ACCRA, Ghana
MIAMBA ya Asante Kotoko ya Ghana, imetangaza kuwa wamekamilisha usajili wa kiungo wa Brazil, Fabio Dos Santos Gama kuelekea msimu wa soka wa 2020/2021.
Wamiliki hao wa rekodi ya Ligi Kuu ya Ghana wamekuwa wakifanya kazi katika dirisha la uhamisho kwa nia ya kukusanya kikosi bora kwa kampeni inayokuja.


“Asante Kotoko inafuraha kutangaza kupatikana kwa kiungo wa kimataifa wa Brazil Fabio Dos Santos Gama”, taarifa rasmi ya klabu, ilisema.


Anajiunga na wachezaji kama Kwame Opoku, Razak Abalora, Yusif Mubarik, Emmanuel Keyekeh, Abdul Latif Anabila, Patrick Asmah, Emmanuel Sarkodie, Andrews Appau, na Evans Adomako Wiredu kama wachezaji wapya waliosainiwa na Kotoko ili kuimarisha kikosi.
Kotoko inajiandaa kutambulisha kikosi tofauti katika msimu wa soka wa 2020/2021 baada ya kuondoa wachezaji 15 kutoka msimu uliopita.


Wakati wa msimu wa 2019/2020, wababe hao wa Ghana walifurahia kampeni nzuri, lakini, hawakuweza kuendelea katika mashindano yoyote ya klabu ya CAF licha ya kushiriki katika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.


Katika miezi michache iliyopita, Kotoko imeachana na wachezaji kadhaa kwa kumaliza mikataba yao ikiwa ni pamoja na Richard Arthur, Collins Ameyaw, Patrick Yeboah, Stephen Ayiku Tetteh, na Empem Dacosta.


Nambari hiyo baadaye iliongezeka baada ya klabu kumfukuza, Matthew Anim-Cudjoe na Justice Blay. Wawili hao walikuwa sehemu ya timu ya Kotoko kwa msimu uliopita lakini hawatakuwa sehemu ya kikosi cha msimu ujao.


Kulinga na taarifa za karibuni ni kwamba wachezaji wengine saba wakiwemo, Martin Antwi, Evans Owusu, Sam Adams, Kelvin Andoh, Kingsley Osei Effah, Douglas Owusu Ansah, na Abass Mohammed wameambiwa hawatakuwa na nafasi katika kikosi cha kocha Maxwell Konadu, msimu ujao.(Goal).