ZASPOTI

MIAMBA ya Ligi Kuu ya Ghana, Asante Kotoko, wameelezea mipango yao ya kumsajili gwiji wa Ghana, Asamoah Gyan kabla ya msimu mpya.
Gyan (33), anatarajiwa kujiunga na Porcupine Warriors kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Ghana.


Inaaminika kwamba kambi ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Sunderland inadai dola 500,000 kabla ya uhamisho huo kukamilika.
“Ni siri ya wazi ambayo Asamoah Gyan ametangaza kuwa angependa kuichezea Asante Kotoko kabla ya kutundika daluga”, Mose Antwi Benefo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa klabu hiyo aliiambia Oyerepa FM.
“Na sisi katika Kotoko tunaamini wakati wa kumpandisha ndani ni sasa.


“Usimamizi [wa klabu] umepewa taa ya kijani kumshirikisha Asamoah Gyan.
“Tumekuwa katika zama ambazo mashabiki wamekuwa wakilala kidogo na tunaamini kuwa kumpata Gyan kutawapa nguvu mashabiki kudhamini michezo yetu.
“Tunaweza kumtumia kama zana ya kuvutia wadhamini na washirika na vile vile kurudisha mashabiki wetu kwenye majukwaa.”


“Kila mmoja anajua uwezo wa Gyan uwanjani. Changamoto pekee tunayokabiliana nayo katika zabuni hii ni fedha”, Benefo aliongeza.
“Hilo ndilo limepunguza majadiliano, lakini, tunatarajia kufikia makubaliano ambayo yatakuwa na faida kwa pande zote mbili.
“Sisi [utawala] tumepewa jukumu la kuifanya Kotoko ijiweze kiuchumi na hiyo ndio tunatafuta kufikia katika kila shughuli,” akaongeza.


Gyan amekuwa hana klabu tangu aondoke NorthEast United ya Ligi Kuu ya India mapema mwaka huu.
Aliendelea kuwakilisha klabu ya Italia, Modena, Rennes huko Ufaransa, Al Ain na Al Ahli Dubai katika Falme za Kiarabu, Shanghai SIPG nchini China na miamba ya Uturuki ya Kayserispor.
Mshambuliaji huyo kwa sasa anasimama kama mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi na mfungaji bora wa muda wote wa Ghana baada ya kucheka na nyavu mara 51 katika mechi 109 za Black Stars.(Goal).