IGP Siro ataka kila mtu awajibike kwa nafasi yake

NA ASIA MWALIM

JESHI la Polisi nchini Tanzania limesema limejiandaa kusimamia sheria ili kuhakikisha zoezi la uchaguzi mkuu linalotarajiwa kufanyika Oktoba 27-28 mwaka huu hapa Zanzibar linakamilika bila kuwepo aina yoyote ya uvunjifu wa amani.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Nyakoro Siro aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza baada ya kukagua gwaride la askari polisi huko katika viwanja vya Ziwani Unguja.

Inspekta Siro alisema Jeshi hilo lipo tayari kwa ajili ya ulinzi wa wananchi na mali zao katika kipindi cha uchaguzi na kwamba lingependa kumuona kila mwananchi anapata na kutimiza haki yake ya msingi ya kupiga kura bila ya hofu ama kikwazo chochote.

Alifahamisha kuwa nchi itakua katika hali ya amani endapo kila mtu katika nafasi yake atatekeleza sheria bila ya kushurutishwa na kwamba jeshi halitomvumilia mtu yoyote atakaejaribu ama kuingilia majukumu na kazi za wengine.

“Sisi kama Jeshi la Polisi tunahakikisha Tanzania itakua shwari na hasa kwa Unguja na Pemba katika kipindi chote kabla, wakati na baada ya uchaguzi”, alisema Siro.

Alieleza kuwa jukumu la kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Taifa lipo kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Tanzania (NEC) na sio viongozi wa vyama vya siasa, hivyo atakaejaribu kutangaza matokeo yasiyo rasmi atachukuliwa hatua za sheria.

 “Kuna baadhi ya wanasiasa wanafanya kazi ya Tume ya kutangaza matokeo jambo ambalo ni kinyume na maadili ya sheria za uchaguzi Tanzania”, alisema.

Aidha aliwataka askari hao kutojihusisha katika suala la uvunjifu wa amani na badala yake wafuate sheria na maadili ya kazi zao zinavyoelekeza.

Mkuu huyo alisema kumekuwa na kauli za baadhi ya kikundi cha watu wanao hamasisha kupiga kura siku ambayo sio rasmi, ambapo kufanya hivyo ni kutotimiza wajibu na sheria hivyo ni uhalifu kama uhalifu mwengine.

“Yoyote asiyehusika atakaekwenda kwenye kituo cha kupiga kura Oktoba 27 mwaka huu, misukosuko itakayomfika asije kulaumu serikali, kwani maelezo yameshatolewa mapema sana”, alisema.