NA KHAMISUU ABDALLAH

SHAHIDI mmoja aliesikilizwa mahakamani amesababisha kesi ya kujipatia fedha shilingi 5,000,000 kuondoshwa mahakamani.

Hakimu Taki Abdalla Habib wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe Septemba 30, mwaka huu, aliiondoa kesi inayomkabili mshitakiwa Zuwena thabit Kassim (28) mkaazi wa Mombasa wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akitoa uamuzi huo mbele ya Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Suleiman Yussuf Hakimu Taki, alisema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kosa kutokana na kuwasilisha shahidi mmoja ambae ni malalamikaji katika kesi hiyo.

Alisema kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuwasilisha mashahidi wengine katika kesi hiyo, hivyo mahakama inamuachia huru mshitakiwa huyo.

“Kesi hii ipo katika hatua ya hukumu, lakini kutokana na upande wa mashitaka kuwasilisha shahidi mmoja mahakama inaifuta kesi hii chini ya kifungu cha 219 (2) cha sheria namba 7 ya mwaka 2004 na mshitakiwa namuachia huru,”alisema.

Mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na shitaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 299 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa Zuwena alidaiwa kuwa bila ya halali kwa njia ya udanganyifu alijipatia fedha taslim shilingi 5,000,000 kutoka kwa Salum Kassim Alawi, baada ya kumdanyanga kuwa atampatia mkopo matokeo yake hakumpatia mkopo wala kumrejeshea pesa zake jambo ambalo ni kosa kisheria.