CONAKRY GUINEA

WATU kumi wameuawa katika ghasia baada ya uchaguzi katika mji mkuu wa Guinea, Conakry, huku taifa hilo likiendelea kusubiri kwa hamu na shauku kuu matokea ya uchaguzi huo wa Oktoba 18.

Hayo yalitangazwa na Wizara ya Usalama ya Guinea ambayo ilifafanua kuwa, raia nane na maofisa usalama wawili waliuawa katika makabiliano makali baina ya waandamanaji na askari polisi jijini Conakry.

Maandamano hayo yaliibuka baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo kutangaza kuwa Rais Alpha Conde (82) anayegombea muhula wa  tata, anaongoza hadi sasa katika mchuano wa urais.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Usalama ya Guinea iliulamu upinzani kwa ghasia hizo za baada ya uchaguzi haswa kwa kuzingatia kuwa, siku chache zilizopita, Cellou Dalein Diallo, kiongozi wa chama cha upinzani cha Union of Democratic Forces of Guinea (UFDG) alijitangaza mshindi wa uchaguzi wa rais.

Diallo alisema hayo, siku moja tu baada ya kufanyika uchaguzi huo na kusisitiza kuwa,licha ya kasoro nyingi zilizougubika uchaguzi na kwa mtazamo wa matokeo kwa mujibu wa masanduku ya kupigia kura.

Hii ni katika hali ambayo, waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika Magharibi (ECOWAS) walipongeza uchaguzi huo katika Jamhuri ya Guinea na kusema kuwa, ulikuwa huru na wa haki.

Tume ya uchaguzi ya Guinea inatazamiwa kutangaza matokeo ya awali baada ya siku tatu.

Mahakama ya Katiba itakuwa na siku nane kutangaza mshindi ambaye sharti apate zaidi ya asilimia 50 ya kura ua uchaguzi huo uingie katika duru ya pili.