TAIFA la Kuwait limetangaza siku 40 za maombolezo ufuatia kifo cha mtawala wa nchi hiyo, Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber al-Sabah aliyefariki Septemba 29 mwaka huu akiwa na umri wa miaka 91.

Kiongozi huyo alifariki majira ya saa 10 za jioni kwa saa za Kuwait na majira ya saa 2 za asubihi majira ya eneo liliopo hospitali ya Mayo iliyopo Rochester mjini Minnesota nchini Marekani.

Inasemekana kwa takriban mwezi mmoja alilazwa katika hospitali hiyo akipawatiwa matibabu kabla ya kufikwa na mauti, hata hivyo kabla ya kulazwa mtawala huyo alikuwa akisumbuliwa na mardhi kwa muda mrefu.

“Kwa huzuni na majonzi makubwa, tunaomboleza kifo cha Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber Al-Sabah”, alisema Sheikh Ali Jarrah Al-Sabah, waziri wa masuala ya ufalme, katika hotuba iliyotolewa kwa njia ya televisheni.

Vyombo vya habari nchini Kuwait zikiwemo radio la televisheni zilirushwa vipindi vyenye maudhui ya maombolezo huku vikirusha hewani visomo vya kur-ani na vipindi vyengine vya dini.

Muda mchache baada ya Sheikh Sabah kufariki mdogo wake wa kiume aitwae Sheikh Nawaf Al Ahmad Al Sabah (83), ametangazwa rasmi kurithi nafasi hiyo na tayari ameshaapishwa kuliongoza taifa hilo lenye utajiri wa nishati ya mafuta.

Wakati akiwa hayupo, Sheikh Nawaf mmoja wa viongozi wakuu wa serikali ambaye ameshikilia nyadhifa za juu kwa miongo kadhaa, zikiwemo wizara za ulinzi na mambo ya ndani alikuka akikaimu nafasi ya mfalme.

Mfalme huyo, alielitawala taifa hilo tajiri kwa mafuta tangu 2006, amefariki nchini Marekani ambako alikuwa akitibiwa, baada ya kufanyiwa upasuaji katika mji wa Kuwait City, taarifa za kina kuhusu ugonjwa wake hazikutolewa.

Kwa hakika kifo cha Sheikh Sabah kinaacha pengo kwa umoja wa nchi za kiarabu ya ghuba ya uajemi inayoshirikiana na nchi za magharibi, kuwa bila ya mmoja wa viongozi wenye uzoefu wakati washirika wa kikanda pamoja na Qatar, Saudi Arabia na Misri wamegawanyika na uhasama ambao mfalme Sabah alijaribu kuupatanisha.

Mtawala huyo alijipatia sifa kama kiongozi shupavu na asietikisika, ambaye aliisaidia nchi yake kupita katika uvamizi wa Iraq wa mwaka 1990, mporomoko wa masoko ya mafuta na machafuko katika bunge na mitaani.

Alitumia ushawishi wake kama mwanadiplomasia wa juu wa nchi hiyo kuunda vita vilivyoongozwa na Marekani dhidi ya uvamizi wa Iraq mnamo mwaka 1991 na kisha kama mtawala alisimamia kurejeshwa kwa uhusiano na Baghdad baada ya kuanguka kwa utawala wa Saddam Hussein.

Katika uhai wake Sheikh Sabah aliunda sera inayotumiwa na taifa hilo hivi sasa ya upatanishi na mpatanishi katika baadhi ya mizozo mibaya zaidi ya kanda ya Ghuba.

Sera hiyo ilimuwezesha kuwa mpatanishi kati ya Baraza la Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba na Iran, na kati ya Saudi Arabia na Qatar, kufuatia uamuzi wa Riyadh mwaka 2017, kukata mahusiano na Doha.

Sheikh Sabah ni kiongozi wa 15 kutoka katika familia ambayo imetawala Kuwait kwa zaidi ya miaka 250, Sheikh Sabah amemudu mizozo ya Kuwait kwa kufanya maamuzi ya uerevu na kutumia mkono wa chuma.

Kama ishara ya heshima aliokuwa nayo mfalme huyo ndani ya migawanyiko ya kisiasa ya kanda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Qatar zimetangaza siku tatu za maombolezo.

“Ulimwengu wa kiarabu na kiislamu yamepoteza mmoja wa viongozi wake muhimu”, alisema rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi katika ujumbe wa Twitter.

Bahrain ilisema kwamba Kuwait imempoteza kiongozi mwenye busara, amir wa binadamu aliependa kilicho bora kwa ajili ya watu.

Pande zinazohasimiana nchini Yemen pia zimetoa heshima pia. Msemaji wa kundi la waasi wa Kihouthi alitweet kuwa waasi hawatosahau mapenzi yake kwa Yemen na umakini wake wa kuzima moto wa vita.

Serikali mjini Baghad ilisema Sheikh Sabah alikuwa ameuweka ukaliaji wa Iraq katika wakati uliyopita na kuunga mkono Iraq mpya baada ya kuondokana na utawala wa Saddam Hussein, akichagua kusimama na taifa hilo dhidi ya ugaidi.

Kiongozi huyo wa Kuwait aliendelea kujihusisha kwa undani katika masuala ya kidunia hadi umri wake wa uzeeni.

Naye Kristin Diwan kutoka taasisi ya Mataifa ya Ghubaya Kiarabu mjini Washington, alisema kifo cha Sabah kitagusa sana, kutokana na umashuhuri wake kama mwanadiplomasia na mpatanishi wa kikanda.

Mabadiliko makubwa ya kisera hayajatarajiwi chini ya mrithi wake, hata baada ya kanda ya Ghuba kupitia mabadiliko makubwa ambapo majirani wa Kuwait, UAE na Bahrain, yaliamua kuanzisha uhusiano na Israel.

“Uongozi wa Kuwait utatoa kipaumbele kwa utulivu wa ndani ya nchi na katika siasa za kikanda. Msisitizo utakuwa kwenye utulivu wa ndani,” alisema Diwan.

“Kutakuwa na mengi ya kusimamia ndani ya nchi wakati ambapo uchaguzi wa bunge ukitarajiwa katika muda wa miezi miwili ijayo”, alisema.

Kuweka sawa uhusiano na Israel ni jambo linalochukiwa sana nchini Kuwait, ambayo kwa sehemu kubwa inaunga mkono msimamo wa kihistoria wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu, wa kudai azimio linalounga mkono harakati za Wapalestina kabla muafaka wa kidiplomasia na Israel.

Katiba ya Kuwait inainisha kuwa mfalme anapaswa kutoka kwenye kizazi cha mwasisi wa taifa hilo, Mubarak al-Sabah, lakini kiti cha ufalme kimezunguka miongoni mwa vizazi vya watoto wake, Salem na Jaber, kwa miongo minne.

Mbali ya kuwa Kuwait kama zilivyo nchi nyingine wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (PGCC) inaongozwa kiukoo, lakini nchi hiyo ina bunge lenye nguvu ya kisiasa.

Bunge la Kuwait lina mamlaka ya kusaili na kuwafuta kazi mawaziri pia lina nguvu ya kufutilia mbali amri na dikrii ya mfalme wa nchi hiyo kupitia thuluthi mbili ya kura za wabunge.

Kuwait ni moja ya nchi za Kiarabu ambazo si tu kwamba hazijakubaliana na suala la kurejesha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel bali zinaunga mkono Palestina mkabala wa jinai za utawala huo wa kigaidi.

Kabla ya kuwa mfalme 2006, Sheikh Sabah alikua waziri wa mambo ya kigeni kwa miaka 50 na kuleta uwiyano katika uhusiano na majirani wakubwa wa Kuwait.

Mnamo mwezi Agosti mwaka jana 2019, serikali ya Kuwait ilitangaza kuwa Sheikh al-Sabah anaugua ugonjwa ambao haukutajwa na kwamba alilazimika kulazwa hospitalini.

Mwezi Julai mwaka huu 2020, Amir huyo wa Kuwait alipelekwa mjini Rochester, katika jimbo la Minnesota nchini Marekani kwa ajili ajili ya matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji.