NCHI zenye uwezo mkubwa kiuchumi au kama zinavyojiita nchi zilizoendelea zimekuwa zikipigania kupata ushawishi barani Afrika.

Katika miaka ya hivi karibuni waafrika wamekuwa wakiwaona viongozi kutoka katika nchi zao wakialikwa kuhudhuria msururu wa makongamano na mikutano.

Aghlabu makongamano na mikutano hiyo hupewa majina yenye maudhui yanayolenga bara la Afrika, yanayoandaliwa sehemu mbalimbali duniani ambayo yanatangazwa kama ushirikiano wa kimaendeleo utakaofaidi pande zote mbili.

Kwa mfano katika mwaka 2019, Japan, Urusi na China ziliwaalika marais na wakuu wa serikali za Afrika kutoka nchi 15 wakifanya mikutano na kuzungumza kile kinachoitwa ushirika na Afrika.

Mbali nchi hizo, viongozi wa Afrika pia walihudhuria kongamano la uwekezaji lililofanyika nchini Uingereza, huku pia mikutano kama hiyo ikitarajiwa kufanyika kwa nchi za Ufaransa, Saudi Arabia na Uturuki mwaka huu wa 2020.

Marekani imekuwa ikijitia kupoteza ushawishi wake barani Afrika, lakini mwanadiplomasia wa juu wa nchi hiyo barani Afrika, Tibor Nagy anataka kubadili hali hiyo.

Nagy ana wasiwasi mkubwa Marekani kuipotezea Afrika inaweza kuwa nafasi nzuri kwa China ambayo kwa kiukweli imelizunguuka bara hilo maeneo yote na kuongeza ushawishi wake.

Biashara ya China na bara la Afrika imeifunika Marekani katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na mnamo mwaka 2018 ilikuwa kubwa mara tatu zaidi.

Nagy anasema anataka kubadili mambo na kurejesha ushawishi wa Marekani kwenye bara la Afrika. ”Kazi yangu ni kuhakikisha kuwa kunapobishwa hodi, kuna mmarekani pia,” alisema.

Huku Marekani ikipuuza hata kuteua mabalozi katika baadhi ya nchi za Kiafrika, tofauti na China ambayo imekuwa ikipeleka maofisa wake kwenye nchi za Afrika.

“Nchini Afrika Kusini, China ina mwanadiplomasia wa juu- hii inamaanisha kuwa ni eneo muhimu kwa Beijing,” anasema Lina Benabdallah, mtaalamu wa mahusiano ya China na Afrika katika chuo cha Wake Forest.

Idadi kubwa ya mataifa yanayoibukia kiuchumi kama vile Uturuki na India, nao wanajitutumua kutafuta ushawishi na uwepo wao katika nyanja za kidiplomasia barani Afrika.

Kwa mfano serikali ya India hivi karibuni iliidhinisha mipango ya kufungua ofisi za kibalozi mpya 18 barani Afrika, jambo hilo linaonesha jinsi bara hilo lilivyokuwa na umuhimu kwa nchi hiyo.

Wadadisi na wachambuzi wamekuwa wakijiuliza kuna nini kwenye mikutano hiyo wanayoalikwa kwenye mikutano na mkongamano sehemu mbalimbali duniani kwenye nchi tajiri.

Kuna masuala mengi yenye faida kutoka Afrika ambayo ni muhimu sana kwa mataifa ya yaliyoendelea ikiwemo utajiri wa mchanganyiko wa utajiri wa madini na rasilimali zilizopo barani humo.

Aidha bara hili, lina ardhi nzuri ya kilimo ambayo kiukweli haijatumiwa ipasavyo, hivyo nchi tajiri zinahitaji ushawishi ili kupata fursa ya bidhaa hizo kwa ajili ya malighafi ama chakula katika nchi zao.

Suala jengine ni kwamba Afrika ina takriban nchi 54, hivyo bara hilo lina kura nyingi kwenye Umoja wa Mataifa, hivyo kadiri unavyojisogeza Afrika unajiongezea nafasi ya kupata kura za bara hilo.

Nchi tajiri pia zina hofu kubwa ya uvamizi kutoka kwa makundi yenye itikadi kali kutoka barani Afrika, zina hofu ya uhamiaji wa kiuchumi ambao wanakilimbilia katika nchi tajiri.

“Ipo haja ya ulimwengu kujadiliana na kusaidia kutatua matatizo ya Afrika, ambayo hivi karibuni au baadaye, yatageuka kuwa tatizo la kimataifa”, aliema mwanauchumi kutoka nchini Zambia, Dambisa Moyo aliyeandaa ripoti yake ya mwaka 2018.

“Hakujawahi kuwa na mashauriano ya kina ya kimataifa kuhusu bara la Afrika, licha ya hilo uchumi wa kimataifa unaweza kunufaika pakubwa kutokana na uwekezaji utakaotokana na bara Afrika”, alisema Dk. Moyo.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alikubaliana na hoja hiyo, katika ziara yake ya hivi karibuni nchini Marekani ambapo alinukuliwa akisema kuwa Afrika licha ya kuwa bara ambalo linachangia changamoto ya kiusalama au uhamiaji usiokuwa mpangilio ambao unaweza kudhibitiwa lakini inaweza kutoa nafasi nzuri ya uwekezaji duniani.

Hata hivyo, Kenyatta alionya kuhusu ushindani kutoka kwa China, Marekani, Urusi na mataifa mengine dhidi ya bara hilo unaoendelea kushamiri hivi sasa.

“Nimeshuhudia mashauriano kati ya nchi za magharibi na washirika wao wa Asia na Mashariki ya kati, nahisi ushindani wa kung’ang’ania Afrika, katika visa vingine… kuchukulia Afrika ni kama inaweza kumilikiwa na mtu yeyote mwenye uwezo… Lakini nataka niwaambie kwamba hilo haliwezekani”, Kenyatta aliongezea.

Huku hayo yakiendelea, Afrika ina mpango gani kutokana na usuhuba huu unaozidi kushika kasi kutoka nchi tajiri?

Mwaka 2013, viongozi wa Afrika, chini ya muungano wa Afrika (AU), walikubaliana kuhusu mpango utakaotoa muongozo thabiti wa kushughulikia changamoto inayokabili bara hilo. Mpango huo ulifahamika kama ajenda ya mwaka 2063.

Katika mpango huo kiliwekwa mipango kadhaa ikiwemo, kumaliza vita katika bara hilo, kuboresha miundo mbinu na kuruhusu utangamano huru baina ya watu wa bara hilo.

Mradi mwingine ambao ulifahamika kama African Continental Free Trade Area (AfCTA), ambao unatajwa kuwa mkataba wa biashara huru kwa mataifa ya bara Afrika, unatarajiwa kuimarisha biashara miongoni mwa mataifa ya Afrika.

Wakosoaji, hata hivyo wanasema AfCTA, ambayo itaanza kutekelezwa mwezi Julai, sio suluhisho la changamoto zinazokabili Afrika na kuongeza itakabiliwa na kuhunzi cha sera ya kujilinda na miundombinu duni ya taifa wanachama.