BEIRUT,LEBANON

LEBANON na Israel zitaendelea na mazungumzo yao yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa muda mrefu wa mpaka wa baharini na ardhini.

Duru ya kijeshi ya Lebanon ilisema ujumbe wa Lebanon katika mazungumzo hayo uliwasilisha ramani na nyaraka zinazoonyesha maeneo yanayozusha utata.

Mkutano huo unaoingia duru ya pili ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili, uliandaliwa katika makao makuu ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa katika mji wa mpakani mwa Lebanon wa Naqoura.

Mzozo kati ya Lebanon na Israel unatokana na mbinu tofauti za kutengeneza mipaka kuhusu eneo la bahari linalotumiwa na nchi hizo mbili.

Mzozo huo umeongezeka baada ya ugunduzi wa gesi katika Bahari ya Mediterania, huku nchi zote zikidai umiliki wa hifadhi za gesi katika eneo hilo.