TRIPOLI, LIBYA

SERIKALI ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, jana iliadhimisha miaka 56 ya Siku ya Polisi ya Libya, sherehe iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu Fayez Serraj na maafisa wengine wakuu, kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi ya habari ya Waziri Mkuu.

“Sherehe ambayo ilifanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ni pamoja na maonyesho ya vikosi maalum vya Wizara hiyo, polisi wa wapanda farasi, polisi wa kilimo, ulinzi wa raia, na kilabu cha michezo cha polisi,” ilisema taarifa hiyo.

Akitoa hotuba katika hafla hiyo, Serraj alisisitiza umuhimu wa usalama kwa kujenga nchi na kuleta maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.

“Sherehe ya leo inakuja baada ya uchokozi uliolenga mji mkuu na miji mingine kushindwa,” Serraj alisema.

“Ushindi ambao umepatikana umekamilika ila amani ya dhati bado hatujafikia kwa hivyo, tuko tayari na tunajilinda,” aliongeza.

Serikali inayoungwa mkono na UN na jeshi hasimu lenye makao yake mashariki walikuwa katika vita vikali vya silaha kwa zaidi ya mwaka mmoja katika mji mkuu wa Tripoli na vitongoji vyake  kabla ya jeshi lenye makao yake mashariki kuondoka kutoka magharibi mwa Libya hivi karibuni.

Waziri huyo wa Ulinzi wa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa Salah Al-Namroush Alhamisi alitoa maagizo kwa vitengo vya jeshi la magharibi kubaki macho, baada ya kupata habari juu ya uwezekano wa shambulio la jeshi la makao makuu huko katika miji ya magharibi.