TRIPOLI,LIBYA

WIZARA ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya imelaani matamshi ya rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na Uislamu na kumtaka afanye haraka kuwaomba radhi Waislamu duniani.

Mohamed al Qablawi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya alisema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na mtandao wa habari wa al Arabi 21 na kuongeza kuwa, matamshi yasiyo ya heshima ya rais wa Ufaransa yamezidisha chuki na hasira dhidi yake na bila ya shaka ametoa matamshi hayo ili kujinufaisha kisiasa katika chama chake.

Vile vile alikumbushia hukumu ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu iliyotolewa mwaka 2018 ambayo ilisisitiza kuwa, kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW si sehemu ya uhuru wa kujieleza na kumtaka Macron afute kauli zake za kichochezi na awaombe radhi haraka Waislamu kote ulimwenguni.

Kabla ya hapo pia Baraza Kuu la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ililitaka  shirika la mafuta la Marathon la nchi hiyo livunje mkataba wake na shirika la mafuta la Total la Ufaransa, kama sehemu ya kuonesha hasira za Waislamu kwa matamshi ya kifidhuli ya rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron.

Mbali na kuwatukana Waislamu, hivi karibuni Macron alitoa matamshi ya kifidhuli na kijuba dhidi ya Uislamu na Bwana Mtume Muhammad SAW akijigamba kwamba Ufaransa itaendelea kusambaza vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume huyo mtukufu.

Ikumbukwe kuwa Waislamu wanaunda takriban asilimia kumi ya wananchi wa Ufaransa.