LIGI Kuu ya Soka ya Wanawake ya Zanzibar ilifikia tamati kwa akinadada wa Women Fighters kutawazwa mabingwa wapya baada ya ngarambe za karibu wiki mbili.

Kukamilika kwa ligi hiyo iliyokuwa na timu nne kulikuwa na changamoto nyingi katika uendeshaji, lakini, nyingi zikiwa ni ukosefu na fedha za uendeshaji sambamba na muamko mdogo kwa soka la wanawake. Tunachukuwa nafasi hii kuzipongeza timu zote zilizoshiriki ligi hiyo na kwa namna zilivyojitahidi kuonesha kile ambacho walikuwanacho kwenye ligi.

Ni ukweli usiopingika kuwa mchezo wa soka ndiyo unaopendwa na mashabiki wengi duniani na ndiyo unaotajwa kupewa kipaumbele zaidi ya michezo mengine.

Pamoja na soka kupendwa, lakini kumekuwa hakuna mwamko mkubwa katika mchezo huo kwa upande wa wanawake, badala yake kumekuwa na hamasa kubwa kwa wanaume pekee.
Kwenye programu nyingi za mchezo wa soka nchini, soka la wanawake limekuwa halipewi umuhimu na wakati mwengine jinsia hiyo hubaguliwa licha ya kuwepo walio na vipaji.

Kwa sasa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), limekuwa na vipaumbele kwenye soka la vijana na wanawake na hiyo imesababisha mashirikisho mengi ya soka kuendesha ligi za wanawake.
Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kwenye sekta ya michezo, kwa sasa imekuwa ikiimarisha soka la wanawake na kwa mara nyengine, ligi ya wanawake imeendelea kuchezwa ambapo jumla ya timu tano zinashiriki.

Pamoja na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kuendesha ligi hii katika wakati mgumu, ipo haja ya kuendelea kuungwa mkono zaidi ili kuiwezesha ligi hiyo kufanikiwa.
Zanzibar Leo tukiwa miongoni mwa jamii ya wanamichezo, tunaona ipo haja ya kuifanya ligi ya wanawake iwe bora na yenye ushindani ili kukuza kiwango cha soka la wanawake.
Katika kila hali, soka la wanawake bado halijawa na nguvu na hiyo imesababisha hata timu za wanawake kutokuwa vizuri na zenye kufahamika.

Hivyo, ipo haja ya kuweka mikakati kwenye soka la wanawake na kupatiwa uungwaji mkono wa kutosha kama ilivyo kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar na tuna imani kuwa ligi hiyo nayo itakuwa na ushindani na bora ili kuiwezesha kutoa timu imara ya taifa itakayopeperusha vyema bendera kimataifa.

ZFF iendelee kupambana katika kuona ligi ya wanawake inachezwa na kupewa aina fulani ya msukumo, licha ya kutambulika kuwepo kwa changamoto kubwa katika suala la wadhamini.
Ni wakati wa wadau wa soka visiwani hapa kuungana na ZFF kuhakikisha ligi ya wanawake inachezwa katika mazingira mazuri na yatakayochochea wasichana wengi zaidi kupenda kucheza mchezo huo.

Wapo wasichana wengi wenye vipaji ambao wanaona aibu kujitokeza, lakini kama kutawekwa mazingira rafiki, bila ya shaka vipaji vingi vitajitokeza na kuunganisha nguvu ya pamoja kwenye soka la wanawake kwa maslahi ya taifa.
Lakini hili pia suala la kuimarisha ligi hiyo linawahusu pia viongozi wa klabu hizo, waongeze juhudi katika ushawishi wa udhamini.

Tunashauri kabla ya kuanza kwa msimu mpya wadau wa soka la wanawake wakutane wazungumze namna ya kutatua changamoto zilizopo kuliko kuendelea kulaumu mamlaka za soka ambazo kimsingi zinafanya jitihada kubwa kwenye kuendeleza soka la wanawake.
Tunaamini mkikutana mtakuja na namna bora ya kuendesha soka la wanawake na kuvutia wadhamini na mashabiki.

Lakini pia ziwepo kozi zenye lengo la kuwajengea uwezo wanawake katika soka kwani soka ya wanawake inakua siku hadi siku.
Imekuwa kawaida wanaume kuongoza soka la wanawake kwenye mambo mbalimbali, lakini wanawake wakipatiwa mafunzo hakuna shaka kuwa wataweza kujiendesha wenyewe.