NA MAUA ALI, TAMISEMI

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheir amewataka maafisa wa vikosi vya idara maalum ya SMZ kuwa chachu ya mabadiliko ya uchumi na kuimarisha ulinzi wa nchi kwa maslahi ya taifa.

Waziri Kheir alieleza hayo katika hafla ya kufunga mafunzo ya askari na maafisa wa idara maalum za SMZ katika ukumbi wa makao makuu ya Kikosi cha Valantia (KVZ) Mtoni, wilaya ya Magharibi ‘A’.

Alisema ipo haja kwa wahitimu wa mafunzo hayo, kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata kuleta mabadiliko kiuchumi na usalama wa raia na mali zao ikiwa ni kutekeleza falsafa ya maendeleo ya uchumi wa buluu na mapinduzi ya kijani.

Alisema falsafa hiyo imekusanya mambo mengi ikiwemo uvuvi wa bahari kuu, mafuta, gesi na utalii hivyo maafisa na wapiganaji hao wanapaswa kujikita ili kuimarisha uchumi.   

Waziri Haji Omar Kheri aliwapongeza wahitimu wa mafunzo hayo kwa ustahamilivu na nidhamu kubwa waliyoonyesha muda wote walipokuwa chuoni.

Katika risala ya wahitimu wa mafunzo hayo iliyosomwa na Kepteni Hussein Mohammed Seif wamesema watayafanyia kazi mafunzo waliyopata kwa kufanya kazi kwa weledi na kuacha kufanya kazi kwa mazowea.

Aidha walimshauri Waziri Kheir kuongeza muda wa yatakapofanyika mafunzo mengine kama hayo, kwani kipindi cha miezi miwili ni kidogo, na kupatiwa fursa za kufanya ziara kwa lengo la kuongeza ujuzi zaidi.

Mafunzo hayo yaliyochukua muda wa miezi miwili, yalivishirikisha vikosi vyote vya idara maalum ya smz, kwa nia ya kuviunganisha kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo ya wananchi, yalianza Agosti 18 mwaka huu na kufungwa rasmi Oktoba 06 mwaka huu.

Katika hafla hiyo, waziri huyo aliwakabidhi vyeti baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo kwa niaba ya wahitimu wenzao 35 akiwemo Naibu Kamishna wa kikosi cha Zimamoto Gora Haji Gora, Kapteni Khamis Tajo, Meja Hussein Ali, SSP Mgeni Kombo na Luteni Kanali Khadija Ahmada Rai.