ABUJA, NIGERIA

MAKUMI ya watu wameuawa katika machafuko na maandamano yanayoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Nigeria.

Katika taarifa iliyotolewa usiku wa jana (24 Octoba), Ofisi ya Rais Muhammadu Buhari ilisema kwa akali raia 51 na maafisa usalama 18 walipoteza maisha katika ghasia na makabiliano baina ya raia na maafisa usalama.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, raia wengine 37 wamejeruhiwa katika maandamano hayo ya fujo ambayo serikali inadai kuwa yamechochewa na magenge ya majambazi yaliyotoka nyara maandamano ya amani ya wananchi.

Hata hivyo alikosolewa vikali ndani na nje ya nchi kwa kadhia ya maafisa usalama kuwapiga risasi na kuua makumi ya raia waliokuwa wakiandamana katika hotuba yake hiyo.

Amri ya kutotoka nje ilitangazwa katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo ili kudhibiti maandamano na machafuko yanayoendelea nchini humo kwa zaidi ya wiki mbili sasa. Raia wa Nigeria wamekuwa wakiandamana kote nchini humo wakipinga ukatili unaofanywa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS).

Akihutubia taifa juzi Alkhamisi, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliwahimiza vijana kusitisha maandamano na kushirikiana na serikali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo.