TEHRAN,IRAN

MAELFU ya Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq wamefanya maandamano ya kulaani hatua ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuunga mkono vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW na matukufu ya Kiislamu.

Maandamano hayo makubwa yalishuhudiwa katika miji mikuu ya Iran na Iraq, Tehran na Baghdad ambapo waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kutaka kususiwa bidhaa za Ufaransa, wameonyesha ghadhabu zao kwa kuvunjiwa heshima Uislamu na matukufu yake.

Nchini Iran, waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ‘Nampenda Mtume Muhammad SAW’, walikusanyika nje ya ubalozi wa Ufaransa jijini Tehran katika barabara ya Neauphle-le-Château.

Mbali na kutaka kutimuliwa balozi wa Ufaransa mjini Tehran, wananchi Waislamu wa Iran katika maandamano hayo walisikika wakiilani Marekani na utawala  wa Israel, tawala ambazo ni vinara wa kuchochea moto wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, waandamanaji walitoa wito wa kuwajibishwa Rais Macron, kutokana na matamshi na misimamo yake ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Hatua ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuunga mkono kitendo cha kifidhuli cha jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW imelaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu, huku kampeni ya kususia bidhaa za Ufaransa katika mataifa hayo ya Kiislamu ikishika kasi.