ABUJA, Nigeria

MAANDAMANO ya nchi nzima dhidi ya ukatili wa polisi yamelikumba taifa la Nigeria kwa siku ya tatu mfululizo. Mtu mmoja anaaminika kufariki juz huku ghasia zikiendelea kati ya waandamanaji na maofisa wa polisi. Huku maandamano hayo yakitarajiwa kuwa ya amani, waandamanaji walishambulia kituo cha polisi na kusababisha kifo cha ofisa mmoja wa polisi.

Polisi walifyatua gesi za kutoa machozi na pia kuwarushia magurunedi waandamanaji hao ambao waliwashtumu maofisa hao kwa kutumia risasi za moto.

Mamia ya watu waliandamana na kutoa wito wa kuvunjiliwa mbali kwa kikosi maalumu cha kukabiliana na waporaji kinachojulikana kama SARS.

Maandamano hayo yalisababisha kusitishwa kwa shughuli katika mji mkubwa wa Nigeria Lagos pamoja na mji mkuu Abuja, na miji mingine midogo.