NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

MAHAKAMANI kuu kanda ya Arusha, Masijala ndogo ya Kazi ,imeamuru kukamatwa kwa magari matatu ya kampuni ya ulinzi ya Knight Support na kupigwa mnada, ili kufidia malipo ya wafanyakazi wa kampuni hiyo yanayofikia kiasi cha sh,million 62,579,860.

Amri hiyo imetolewa jana na Msajili wa mahakama hiyo John Mkwabi,  anayesikiliza shauri la madai namba 73 la mwaka 2020 na kumwamuru meneja wa kampuni hiyo ya ulinzi kukabidhi funguo za magari hayo kwa dalali wa mahakama  ndani ya siku 15  kuanzia sasa.

“Kwa kuwa mahakama imeshatoa oda ya kukamatwa kwa magari hayo ,naagiza meneja wa kampuni ya Knight Support kukabidhi funguo za magari hayo kwa dalali wa mahakama kabla ya Oktoba 16, mwaka huu” Alisema  Msajili.

Awali Ofisa kazi wa mkoa wa Arusha, Emmanuel Mweta, aliieleza mahakama hiyo kwamba shauri lilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya kuomba tarehe ya kuuza magari hayo ambayo ni pamoja na gari Lenye namba T 319 DAJ aina ya Ford( ambulance), Gari aina ya Suzuki namba T 637 BBY na gari aina ya Suzuki lenye namba T706 DED .

Hata hivyo, kutokana na funguo za magari hayo kutopatikana mahakamani iliamua kusogeza mbele na kuagiza funguo za magari hayo zikabidhiwe kwa dalali wa mahakamani.

Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Novemba 3, mwaka huu kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya utekelezaji wa Mnada wa kuuza magari hayo.