NA ABOUD MAHMOUD

WADAU wa michezo visiwani Zanzibar wamesema kuwepo kitabu kinachozungumzia mambo yanayohusiana na mchezo wa soka kutasaidia kuleta mabadiliko na maendeleo yanayohitajika.

Hayo yamesemwa na wadau hao mara baada ya uzinduzi wa kitabu kinachojulikana kwa jina la ‘mwalimu bora wa soka’, kilichozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni.

Walisema walimu  wengi wa mchezo wa soka  hapa nchini hivi sasa hutumia utaalamu wanaoupata wa mafunzo ya muda mfupi na walimu wanaofundisha timu za nje ya nchi.

Walisema wanaamini kuzinduliwa kitabu hicho kutasaidia walimu pamoja na wachezaji kupata taaluma, ambayo itasaidia kuwapa mwangaza mzuri na kuhakikisha soka la Zanzibar linakua siku hadi siku.

“Nimefurahi sana kuona leo Zanzibar tumeweka historia ya kuwa na kitabu cha mchezo wa soka tena kimeandikwa kwa lugha yetu ya Kiswahili, hii itasaidia kuinua soka letu tena kwa zaidi na wachezaji na walimu wataweza kujifunza mbinu mbali mbali za mchezo huu,”alisema mchezaji mkongwe Salum Mkweche.

Mkweche  alieleza kuwa anaaamini kuwa kitabu hicho kitakua chachu ya kuleta maendeleo ya soka, kutokana na uandishi uliotumika na kuweza kuwajengea ufanisi wanasoka.

Nae mchezaji wa zamani Haroub Ali alisema ni vyema wanasoka wa hivi sasa hususan makocha wa mchezo huo, kuhakikisha wanakitumia kitabu hicho katika kuwajengea uwezo wachezaji kwa misingi ya kuupandisha hadhi mchezo huo na nchi ujumla.

Haroub ambae ni baba mzazi wa aliekuwa mchezaji wa klabu ya Yanga Nadir Cannavaro, alisema anaamini kitabu kitatumika kama  kilivyokusudiwa wachezaji wa Zanzibar wataweza kuuzika katika nchi mbali mbali duniani kutokana na uzoefu walioupata .

“Kitabu kizuri kimeandikwa kwa mpango uliopangika naamini Gulam amefanya kazi ambayo itaweza kulisaidia taifa la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia ramani ya soka,”alisema Haroub.