NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Haki ya Afrika Mashariki imetupilia mbali shauri la Rashid Salum Adily na wenzake 39,999 waliokuwa wakipinga uhalali wa vifungu na hati za makubaliano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza na wandishi katika Afisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jana jijini hapa, Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Pascol Malata, amesema kuwa shauri hilo limetolewa uamnuzi wake septemba 29 (juzi) mwaka huu, kwa njia ya video ( VIDEO CONFERENCE).

Alisema Novemba 2, mwaka 2016, Rashid na wenzake 39,999 walikwenda kwenye mahakama hiyo kufungua shauri namba tisa ya mwaka 2016, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Katibu Mkuu kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakihoji na kupinga uhalali wa vifungu na hati ya makubaliano ya Muungano Tanganyika na Zanzibar.

Alieleza  sababu hizo ni pamoja na hati ya Makubaliano inayodaiwa kusainiwa Aprili 26, mwaka 1964 baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar haipo na ni batili.

Alisema hati ya makubaliano inayodaiwa kusainiwa Aprili 26, 1964 baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar haijawahi kuridhiwa wakati wowote ule na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Aidha, alisema uwepo wa Jamhuri ya Muungano ni batili kwa sababu umetokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambao haujawahi ridhiwa na pande zote mbili za Muungano.

Alisema hivyo waliiomba Mahakama itoe tamko la kubatilisha Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao umetokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Alifafanua kuwa, kwa upande wa serikali ambao ni wajibu maombi, waliwasilisha majibu ya utetezi juu ya uhalali wa kisheria wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na mapingamizi ya awali ya kisheria.

Alitaja mapingamizi hayo ni pamoja na Mahakama ya Afrika Mashariki haina mamlaka kisheria kusikiliza hoja za kupinga uwepo wa Taifa la Tanzania lililotokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

“Madai yamewasilishwa nje ya muda uliowekwa na ibara ya 30(2) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 1999”, alisema.