NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema  kazi ya urais sio ya majiribio na mchezo bali ina vigezo vyake katika kuwaongoza watanzania bila kujali dini rangi wala kabila.

Majaliwa alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni wa kuwaombea kura wagombea wa CCM uliofanyika katika uwanja wa mpira Cairo Kiwengwa wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema, wanatanzania wamepewa fursa kikatiba Oktoba 28 ya kutafuta na kuamua kuchagua viongozi wanaowataka ili kupata rais atakaeongoza watanzania mwenye tofauti ya dini, kabila mwenye kuwaunganisha watanzania na kuwaletea maendeleo na sio wengine bali ni viongozi wanaotokana na CCM.

Aidha, alisema ni lazima rais awe na uwezo wa kutunza tunu za Taifa na kuitunza amani ya nchi ambapo kazi hiyo inaweza kufanywa na CCM na sio mwengine.

Alisema ni jambo la msingi kwa wananchi kutochagua kiongozi anaewachonganisha watu, kuwadanganya watu bali kupata rais mwenye uwezo wa kuwatumikia watanzania.

“Tunahitaji kupata rais mwenye uwezo kuongoza watu zaidi ya milioni 60 na kuzikusanya rasilimali za nchi pamoja na kuona zinarudi kwa wanyonge na kuunda serikali itakayoisimamia na kuwajibika kwa watanzania,” alisema.

Alisema ni wakati muafaka kwa wananchi wa Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla kufanya maamuzi sahihi kwani nchi inataka maendeleo na sio jambo jengine.

Alisisitiza kuwa Tanzania inataka kiongozi atakaepambana na walarushwa na mafisadi ambao wataosababisha kuzorotesha maendeleo ya Taifa la Tanzania.

“Tunataka kiongozi msafi na muadilifu sio mla rushwa, tunataka kiongozi anaeheshimu misingi na sheria za nchi nawasihi sana mtulie katika kuchagua Rais wa Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.