BAMAKO,MALI

MAOFISA nchini Mali wamewaachia huru wapiganaji 180 wenye itikadi kali za Kiislamu kutoka kwenye gereza la Bamako na kuwapeleka kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa hizo zilizusha uvumi kwamba huenda mwanasiasa maarufu wa upinzani Soumaila Cisse anayeshikiliwa na wapiganaji wa jihadi anaweza kuachiwa baada ya kuwepo kifungoni kwa muda wa miezi sita.

Inaaminika kuwa wanamgambo waliomteka Cisse mwishoni mwa mwezi Machi, wanataka mpango wa kubadilishana wafungwa na Serikali ya Mali.

Wafungwa 70 waliachiliwa huru na wengine 110 waliachiliwa huru jana.

Wakati anatekwa, Cisse, mwenye umri wa miaka 70 ambaye aliwahi kugombea urais wa Mali mara tatu, alikuwa akifanya kampeni kabla ya uchaguzi wa wabunge karibu na mji wa Timbuktu.

Mlinzi wake aliuawa katika shambulizi na uthibitisho pekee kwamba bado yuko hai, ni barua aliyoiandika kwa mkono wake na kutolewa mwezi Agosti.