NA MWANTANGA AME

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, amewaongoza wanawake wa Chama cha Mapinduzi kuiombea dua nchi ikiwa inaingia katika uchaguzi Mkuu, unaoanza leo katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Mama Mwanamwema alishiriki katika dua hiyo iliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ilifanyika katika ukumbi wa Ofisi Kuu ya Chama, Kisiwandui, ambayo iliwahudhuriwa na wanachama wa chama hicho na wananchi wa Zanzibar.

Dua hiyo, ilifanyika kuliombea taifa ambalo leo limeingia katika uchaguzi mkuu ambao utatoa nafasi kwa wananchi wa Zanzibar kuchagua viongozi mbali mbali wakiwemo Wagombea wa Urais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

Uchaguzi huo, unafanyika ikiwa ni baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kumaliza muda wake wa uongozi ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Dua hiyo, pia ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali na chama, akiwemo, Mke wa Mgombea wa Chama cha Mapinduzi, Maryam Hussein Mwinyi, Mama Asha Bilal, Zakia Bilal, Asha Shamsi na Balozi Amina Salum Ali, pamoja na makundi ya vijana na wanawake na wazee wa chama hicho.

Uchaguzi Mkuu unafanyika kesho kwa wananchi wote ambapo leo utafanyika kwa kuyahusisha makundi maalum yalioyoruhusiwa kisheria.