NA MWANAJUMA MMANGA

BARAZA la Manispaa Magharib ‘A’ limesema linampango wa kuimarisha shamba la Selemu kwa ajili ya kuotesha miche mingi ya zao la Mnazi na Mikarafuu.

Mkurugenzi wa baraza hilo, Amour Ali Mussa, alisema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko ofsini kwake Mwera.

Alisema iwapo mazao hayo yatazalisha na kuongezewa thamani kutaweza kusaidia wananchi pamoja na kutaondokana na kuwepo kwa adimu ya mazao hayo kwani  zaidi ya miche 2000 ya mnazi na mikarafuu itapandwa mwaka ujao.

Aidha alisema serikali imedhamiria kulirejesha upya zao hilo hapa Zanzibar, ili kuondokana na kuangiza nje ya nchi na wananchi kufaidika kwa kiasi kikubwa.

“Ninaimani kubwa mazao haya tukilizalisha kwa wingi hapa petu tutapunguza tatizo la zao la nazi, lakini pia tutapunguza ukataji wa miti hii kuipoteza kabisa” alisema.

Alifahamisha kuwa zao la nazi na karafuu ni mazao makuu kama pilipili hoho ambayo yanabei kubwa hapa Zanzibar, hivyo ni vyema wananchi kuyaendeleza na kuyasimamia katika kuyatunza.

Alisema pia baraza limejipanga kuboresha sekta ya kilimo mwakani katika eneo hilo, ili kuhakikisha kilimo kinaimarika ndani ya wilaya hiyo.

Hivyo, amewataka wananchi kupenda kulima zaidi mazao hayo ili kutasaidia kuepuka tatizo la nazi na karafuu.

Alisema ukiacha mazao hayo lakini pia watahamasisha wananchi kutunza mazingira katika maeneo ya kilimo na kuwataka kutochimba ovyo mchanga katika maeneo hayo ili kuepusha mabadiliko ya tabia nchi.