Na Zubeir H. Zubeir

UNUNUZI wa Umma unaweza kuwa ni nyenzo ya kurahisisha kufikia mipango ya maendeleo ya kitaifa au kudhoofish maendeleo. Taarifa kadhaa zinaonesha changamoto zinazolikabili eneo la ununuzi wa umma katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa.

Kwa mfano Tanzania, matumizi ya rasilimali fedha kupitia ununuzi wa umma katika maeneo ya bidhaa na huduma yanachukua kipaumbele cha kwanza baada ya mishahara. 

Aidha, wastani wa asilimia 80 hadi 85 ya bajeti ya Serikali hutumika kila mwaka katika ununuzi wa umma hususan kwenye upatikanaji wa bidhaa, kandarasi za ujenzi na huduma.

Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG) kati ya mwaka wa fedha wa 2017/18 hadi 2019/20 baadhi ya taasisi zilizokaguliwa zilionesha kutumia kiasi cha shilingi 70.787 hadi 83.74 bilioni kwa kipindi cha miaka hio, wastani wa shilingi 5.848 kwa mwaka katika ununuzi wa umma.

Taarifa hiyo inathibitisha kuwa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali zinatumika katika ununuzi wa umma.

Pamoja na Serikali kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika ununuzi wa umma Zanzibar, eneo hili bado halikupewa kipaumbele kinachostahili, kwa takribani miaka 15 kuanzia mwaka 2005 ambapo Zanzibar tulianza kutekeleza Manunuzi kwa kutumia Sheria Nambari 9 ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma ya mwaka 2005 hadi mwaka 2019 tukiwa tunatumia Sheria mpya Namba 11 ya mwaka 2016. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekua ikitekeleza kazi za Manunuzi kwa kuzingatia Sheria hizi ambazo kiujumla zimeleta mabadiliko kwa kiasi Fulani katika sekta kulingana na mahitaji ya sekta hii kwa wakati tulionao.

Katika kipindi cha miaka Mitano (5), kuanzia mwaka 2016 hadi 2020 ambapo tunatekeleza kazi za manunuzi kwa kutumia Sheria mpya, kumewako na mabadiliko ya kiutendaji ya ununuzi wa umma.

Mabadiliko haya ya sheria ya ununuzi wa umma pamoja na mambo mengine yanatokana na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Mamlaka ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma Zanzibar ipo katika jitihada za kuandaa sera na misingi ya Taifa ya ununuzi wa umma Zanzibar ambayo inaendelea kuandaliwa.

Sera pamoja na misingi hiyo zitakapokamilika zitakua nyenzo muhimu sana katika kuhakikisha rasilimali za viziwa vya Zanzibar zinatumika kwa manufaa mapana ya wazanzibari kulingana na mipango ya taifa ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Zanzibar.

Dira ya sera ya Taifa ya ununuzi wa umma inataja kujenga ushindani, usawa, uwazi, wajibikaji na ubora wa kazi katika mfumo wa ununuzi wa umma nchini.

Pamoja na changamoto za ununuzi wa umma katika matumuzi yasiyo sahihi ya gharama za huduma na bidhaa, muda, mawanda na ubora, panapaswa kuwepo uzalendo kwa watumishi wanaosimamia eneo hili.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amekua akikemea vikali tabia za baadhi ya watendaji wasiokua waaminifu katika sekta hii na kuwataka watendaji hao kufanya kazi kwa misingi ya kizalendo ili kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na ubora wa huduma zinazotolewa na serikali.

Tofauti ya shilingi 1,000 katika bei za bidhaa na huduma zinazonunuliwa kupitia taratibu za Manunuzi ya Umma, inaweza kutumika katika kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma katika maeneo mengine.

Eneo la ununuzi wa umma halipaswi kuwa kichaka cha wizi na ubadhirifu wa mali ya umma na badala yake liwe ni eneo la weledi na uaminifu uliotukuka ili kuleta tija iliokusudiwa.

Ili kutekeleza hili kwa ufanisi, ni vyema Serikali kupitia Mamlaka ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma Zanzibar ikatengeneza mfumo imara wa ufuatiliaji na usimamizi wa ununuzi wa umma kabla na baada ya kukamilika kwa mikataba inayoingiwa katika taasisi zote za Serikali.

Aidha, taasisi nunuzi yoyote ya Serikali isiruhusiwe kufanya ununuzi wa huduma au bidhaa bila kuhakikisha ina fedha ya kulipia huduma husika kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Biashara na Viwanda itoe bei elekezi kwa bidhaa na huduma zote zinazohitajika katika kutekeleza kazi mbali mbali katika taasisi za serikali ili kutimiza malengo ya Serikali waliojipangia.

Kufanya hivyo kutaondosha moja kwa moja upotevu wa fedha za serikali usio wa lazima kwa kuwa kila mahitaji yatakua na bei elekezi na taasisi nunuzi watalazimika kununua kwa kufuata bei hizo.

Watendaji wa Serikali wanapaswa kuwa wazalendo, wenye kuipenda nchi yao na kutanguliza maslahi ya visiwa vyetu na wananchi wake mbele badala ya maslahi binafsi.

Taasisi za Serikali zisaidiane katika utekelezaji wa majukumu, mfano shirika la nyumba la Zanzibar (ZHC) litumie wakala wa majengo Zanzibar (ZBA) katika kusanifu majengo na kusimamia, na kuitumia Kampuni ya Serikali ilioanzishwa kwa kazi za ujenzi.

Kuwatumia wakala wa Ulinzi wa JKU katika kazi za ulizi badala ya kukimbilia kulindwa na taasisi za kiraia, kuvitumia vikosi vya SMZ katika kufanya kazi ambazo kiufundi na kiuzoefu wanaweza kuzifanya kwa gharama nafuu,kuitumia ofisi ya Wakala wa Serikali wa Uchapaji (ZAGPA) na kuitumia Karakana Kuu ya Serikali katika matengenezo ya Magari ili kunusuru upotevu wa pesa usiokua wa lazima na kutekeleza kwa vitendo malengo yaSerikali ya kuazisha Mawakala au taasisi hizo na mifano mingine inayofanana hii.

Mwisho, napenda kuchukua nafasi hii kutumia haki yangu ya kikatiba nikiwa kama mwananchi na Mzanibari halai chini ya Ibara ya 18(1) ya katiba ya Zanzibar Toleo la mwaka 2010 kuishauri Serikali iweke viwango vya kutoa kandarasi kwa wageni na wazawa kwa maana ya kulazimisha kandarasi zote wanazopewa wageni.

Aidha kushirikiana na wazawa kwa lengo la kuboresha uzoefu na teknolojia kwa kandarasi wa Zanzibar pamoja na kuwaangalia watu wa makundi maalumu katika fursa za kimanunuzi kwa lengo la kuwasaidia katika kuimarisha hali zao za kiuchumi na kupunguza umasikini.

Pia mikataba ya ununuzi kwa kandarasi za huduma na bidhaa ibainishe rasilimali za kuagiza nje kwa lengo la kuimarisha sekta ya viwanda hapa visiwani Zanzibar na uchumi wa ndani.