NA KIJA ELIAS, MOSHI

MKUU wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Rajab Kundya, amewataka Maafisa Biashara na Tehama, kujiepusha na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma saidizi kwa wananchi, ili kuonesha matokeo chanya katika lengo lililokusudiwa na serikali.

Alhaji Kundya,  alitoa wito huo jana, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa maafisa biashara na Tehama yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, ambapo yanajumuisha maafisa biashara kutoka Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Alisema Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imekamilisha kutengeneza mfumo mpana wa usajili kwa njia ya mtandao (ORS) mfumo ambao utatatoa huduma zote kwa njia ya mtandao, ikiwemo usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara pamoja na huduma zote.

““Naomba kutoa wito kwenu washiriki wa mafunzo haya, wote watakaopata bahati ya kupatiwa mafunzo haya siku za baadae nendeni mkatoe huduma hizi saidizi kwa wananchi kwa weledi na uaminifu mkubwa, jiepusheni kabisa na vishawishi au kupokea rushwa katika utoaji wa huduma hii ili mafunzo haya yaoneshe matokeo chanya,”alisema DC Kundya.

Kwa upande wake Ofisa Rasilimali Watu kutoka katika Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Tulizo Mpina, alisema Brela, imetoa mafunzo hayo kwa ajili ya kuwajengea uwezo maafisa biashara baada ya kutoka kwenye mifumo ya usajili ya zamani na kuwa na usajili wa njia ya mtandao.

“Mafunzo haya kwetu sisi ni endelevu lengo likiwa ni kuwajengea uwezo maafisa biashara, tunafanya hivi kwa sababu maafisa biashara wa halmashauri na maafisa tehama ndiyo wanawajibika moja kwa moja karibu na wananchi,”alisema.