WASHINGTON,MAREKANI

BARAZA la Seneti nchini Marekani limemuidhinisha  Amy Coney Barrett kuwa jaji wa Mahakama ya Juu baada ya kupata kura 52 dhidi ya 48 huku Seneta mmoja pekee wa chama cha Republican akihamia upande wa wapinzani Democrats.

Hatua ya kuidhinishwa Barrett ni ushindi kwa Rais Donald Trump, ambaye alimteuwa jaji huyo muda mfupi baada ya kifo cha jaji wa zamani shujaa wa Kiliberali Ruth Bader Ginsburg mwezi uliopita.

Warepublican walichukua hatua ya haraka kuijaza nafasi hiyo kabla ya uchaguzi wa rais wiki ijayo.

Wademocrat wanahofia Barrett ataifanya mahakama hiyo yenye majaji tisa kuegemea zaidi upande wa kihafidhina, ikiwa ni pamoja na masuala kuhusu ulinzi wa huduma za afya, utoaji mimba, haki za mashoga na udhibiti wa bunduki.

Mahakama ya Juu ya Marekani tayari imemuapisha Barrett na kumruhusu kuanza majukumu yake.