WASHINGTON,MAREKANI

WIZARA  ya Sheria ya Marekani imesema kwamba wanamgambo wawili wa zamani wa kundi la Islamic State wamefunguliwa mashitaka kwa kuhusika katika mauaji ya raia wanne wa Marekani nchini Syria.

Pia walidaiwa kuhusika katika vifo vya mateka wawili raia wa Japani.

Washukiwa hao ni Alexanda Kotey na El Shafee Elsheikh ambao walinyang’anywa uraia wa Uingereza.

Wizara hiyo inasema wawili hao wanakabiliwa na mashitaka ya utekaji uliosababisha vifo katika visa vya raia wanne wa Marekani, wanaosadikiwa kuuawa mwaka 2014 au 2015.

Kadhalika wizara hiyo inasema wawili hao walihusika katika mauaji ya raia wasiokuwa Wamarekani wakiwemo raia wawili wa Japani.

Wawili hao inaonekana ni Goto Kenji na Yukawa Haruna waliouawa mwaka 2015.

Kotey na Elsheikh walizuiliwa nchini Syria mwaka 2018. Walikuwa wameshikiliwa kwenye kizuizi cha kijeshi nchini Marekani tangu mwaka jana.