NEW YORK, MAREKANI

WIZARA  ya Sheria nchini Marekani inasema maofisa sita wa ujasusi wa Urusi wameshitakiwa kwa kufanya mipango ya mfululizo wa udukuzi wa mtandaoni duniani ukilenga taasisi za Serikali na mashirika mengine kati ya mwaka 2015 na 2019.

Maofisa hao wanakabiliwa na mkururo wa mashitaka yakiwemo kula njama ya kufanya hila na utapeli kwenye kompyuta, utapeli wa fedha mtandaoni na wizi ulioongezeka wa utambulisho.

Maofisa wanasema udukuzi huo ulisababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni kumi.

Kwa mujibu wa mashitaka,watuhumiwa walidukua Mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi ya mwaka 2018 nchini Korea Kusini na kufuta data kutoka kwenye maelfu ya kompyuta zinazohusiana na mashindano hayo.

Maofisa wa Serikali ya Uingereza walioshiriki katika uchunguzi huo walisema udukuzi pia uliyalenga mashirika yaliyohusika katika Mashindano ya Olimpiki na Paralimpiki ya mwaka 2020 kabla ya kuahirishwa.

Maofisa wa Wizara ya Sheria nchini Marekani wanasema muda wa kuwashitaki watuhumiwa hao hauhusiani na uchaguzi ujao wa urais nchini humo.