NA KHAMISUU ABDALLAH

KUTOFIKISHWA kwa mashahidi kwa kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa Saleh Mohammed Saleh (38) mkaazi wa Bububu kijichi wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja imeisababishia mahakama kuliondoa shauri hilo.

Hakimu Suleiman Said Suleiman, aliliondoa shauri hilo Septemba 29 mwaka huu baada ya kesi hiyo kukaa muda mrefu bila ya kusikilizwa shahidi.

“Kutokana na kesi hii ipo kwa muda mrefu na hatuna hata siku moja hatusikiliza shahidi mahakama inaamuru kuiondoa mahakamani kesi hii na mshitakiwa aachiwe huru,” alisema Hakimu Suleiman.

Kabla ya mahakama kutoa uamuzi huo upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Mohammed Haji Kombo, ulidai kuwa aujapokea shahidi na kuomba kesi hiyo kuhairishwa na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa. 

Mshitakiwa huyo awali alikuwa akikabiliwa na shitaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 305 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa Julai 29 mwaka 2013 saa 11:00 asubuhi huko Bububu wilaya ya Magharibi ‘A’ alijipatia fedha taslim shilingi milioni 2,800,000 kwa lengo la kumuuzia kiwanja Sheha Ali Said huku akijua kwamba kiwanja hicho sio chake na wala kumrejeshea pesa zake jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo kwa mara ya mwanza Januari 21 mwaka huu alilikataa ndipo upande wa mashitaka ulipodai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika.