NA MARYAM HASSAN

KITENDO cha mashahidi kudharau hati za wito zilizotolewa na mahakama ya mkoa Mwera kumepelekea kesi ya Dhamir Haji Juma (27) mkaazi wa Bwejuu kuahirishwa.

Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Shumbana Mbwana ameiambia mahakama kuwa inaonekana kuwa mashahidi hao hao wamepokea hati za wito, lakini hawana taarifa kwanini wameshindwa kufika mahamani.

Alisema hatu hiyo, inaonesha ni dharau kwa sababu sheria inaruhusu kama watakuwa na dharura wanatakiwa kuwasilisha taarifa.

Hivyo aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikiliza mashahidi kwa sababu shahidi hawajafika mahakamani.

Mshitakiwa huyo, anakabiliwa na kosa la kupatikana na dawa za kulevya analodaiwa kutenda Febuari 17, mwaka jana majira ya saa 6:06 za usiku huko Binguni wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa alipatikana na mkoba mweusi ndani yake mkiwa na furushi moja la majani makavu lililofungwa karatasi ya gazeti misokoto 45, kila mmoja mkiwa umefungwa karatasi ya kaki na nyongo 59 zinazosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu wa 95.027 jambo ambalo ni kosa kisheria.

Hivyo Hakimu wa mahakama hiyo, Khamis Ali Simai ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 19, mwaka huu na amewaonya mashahidi.