NA MARYAM HASSAN
WAZIRI wa Katiba na Sheria Khamis Juma Mwalim, amehimiza kudumishwa amani na kwamba mtu yeyote ataechafua amani atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Hayo aliyasema wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa maimamu wa misikiti wa mikoa mitatu ya unguja katika ukumbi wa Ofisi ya Mufti mkuu wa Zanzibar, Mazizini.
Alisema masheikh na maimamu nchini wana nafasi kubwa ya kuwahamasisha waumini wao kuhakikisha wanatunza amani na utulivu uliopo nchini ili kuchochea kasi ya maendeleo ya jamii.
Alisema kwa kuwa wao wana nafasi kubwa katika jamii, ni vyema wakatumia vyema majukwaa yao kuhubiri amani ili wanajamii wazingatie wanachohubiriwa.
“Nakuombeni mkazitumie aya zote za qur-ani zinazozungumzia amani na mzitilie mkazo, wala msione taabu kuzitolea mfano nchi ambazo ziliichezea amani hatimae sasa wanahangaika kuirejesha lakini wanashindwa kama ilivyo Libya,” alisema.
Mapema katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema Ofisi ya Mufti imepanga kuonana na viongozi hao kwa lengo la kubadilishana mawazo juu ya umuhimu wa kuimarisha amani na utulivu katika maeneo yao.
Alisema kwa kuwa viongozi hao ni wadau muhimu ambao wapo chini ya Ofisi ya Mufti hivyo ni vyema kuwa nao karibu katika kuwakumbusha masuala mbali mbali ya duniani na akhera.
Akiwasilisha mada Sheikh Khamis Mohammed, alisema wajibu wa viongozi wa dini ni kuhakikisha kuwa kila mwanadamu au kiumbe chochote kinachoishi duniani kinahitaji amani na utulivu.
Akitoa mfano juu ya namna amani ilivyovunjika wakati wa Nabii Adam, alisema Nabii huyo alikuwa na uzao wa watoto pacha yaani kike na kiume.
“Katika uzao huo watoto wake Habil na Qaabil walitakiwa kila mmoja amuoe ndugu wa mwenziwe, lakini hali ilikuja tofauti kwa sababu Qaabil alikataa kumuoa ndugu wa Habil eti tu kwa sababu mbaya jambo ambalo lilipelekea kuvunjika kwa amani kwani Qaabil alimuua kaka yake,” alisema Sheikh Khamis.
Alisema kupitia mfano huo ni wazi kwamba ipo haja ya kutumia busara na hekma kwa ajili ya kuhubiri amani ili kuepusha machafuko ambayo yana madhara kwa jamii.