NA ABOUD MAHMOUD

MASHINDANO ya kuwania kombe la Dulla Sunday yamesitishwa mpaka umalizike uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika leo nchini.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, mratibu wa mashindano hayo, Abdullah Thabit ‘Dulla Sunday’ alisema wameamua kusitisha ili shughuli za uchaguzi zipite bila usumbufu.

Alisema kwa vile washiriki wa mashindano hayo ni wapiga kura wameona shughuli hizo wazisitishe na kuwapa nafasi washiriki wa mashindano hayo pamoja na mashabiki kupiga kura.

“Mashindano haya hivi sasa yamepamba moto lakini kutokana na hali ya nchi hivi sasa kukabiliwa na uchaguzi mkuu tumeamua kusitisha mpaka harakati hizi zitakavyomaliza na sisi tutarudi uwanjani,”alisema.

Sunday aliwashauri washiriki wa mashindano hayo pamoja na wanamichezo kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kupiga kura kwa amani na utulivu ili waweze kurudi tena uwanjani bila kuwepo kwa matatizo.

“Nawaomba wanamichezo wote leo waende kupiga kura na watumie amani iliyokuwepo nchini iendelee kwani bila ya amani hakuna michezo itakayochezwa wala jambo lolote kufanyika hapa nchini,”alisema.

Mratibu huyo alifahamisha kwamba ili nchi iweze kuwa na maendeleo ikiwemo kukua kwa sekta ya michezo ni vyema kudumisha amani na utulivu.