NA ZUHURA JUMA

MASHIRIKA binafsi nchini yametakiwa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuwasaidia wananchi kwa kuwapa elimu itakayosaidia  kuleta maendeleo endelevu nchini.

Akizungumza katika mkutano wa tathmini ya mradi wa Afrika Tunayoitaka,  ulioandaliwa na Shirika la Actionaid Pemba, Katibu Tawala Wilaya ya Micheweni, Hassan Abdalla Rashid, alisema, taasisi binafsi zina mchanago mkubwa katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kufikia malengo iliyojipangia.

“Tunaujua mradi huu na miradi mengine mnayoitekeleza, munatoa elimu kwa wananchi juu ya mambo mbali mbali yakiwemo ya kiuchumi, kujua haki zao, kudumisha amani, kupambana na rushwa, hii itasaidia kupata maendeleo,” alisema.

Alisema Actionaid inaendelea na juhudi za kuisaidia serikali juu ya upatikanaji wa haki kwa wananchi, kupambana na rushwa na utawala bora. Akiwasilisha tathmini hiyo, Mratibu wa shirika la Actionaid Pemba, Severin Mapunda alisema, wananchi wengi hawaujui na wala hawajawahi kuuona mkataba wa demokrasia, uchaguzi na utawala bora (ACDEG), jambo ambalo liliwapa shida wakati wanapokwenda kuwaelimisha.

“Lakini tunashukuru tumepiga hatua, kwa sababu watu wamejua haki zao, kupambana na rushwa pamoja na kudumisha amani na utulivu,” alisema.