LONDON, England
KIUNGO, Juan Mata, amekataa ofa ya pauni milioni 18 kuhamia katika klabu moja ambayo haikutajwa ya Saudi Arabia.
Mata kwa miaka kadhaa sasa amekuwa akitupwa benchi na hajashirikishwa katika mechi ya Manchester United.
Lakini, alishirikishwa katika mechi mbili ikiwemo Kombe la Carabao ambapo alichangia pakubwa katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Brighton na kufuzu kwa robo fainali ya mashindano hayo.

Katika kujaribu kumnasua kwenye hali ya kusugua ubao Old Trafford, inaripoti kuwa Muhispania huyo alikabidhiwa ofa ya pauni milioni 11.5 kuhamia Saudia.
Kulingana na gazeti la Daily Mail likinukuu Shirika la Hispania la AS, ofa hiyo iliongezwa hadi pauni milioni 18, lakini, Mata alikataa kuhama.

Inaaminika kuwa mkali huyo wa zamani wa Chelsea hana hamu ya kuhama na ana matumaini huenda United itashinda taji msimu huu. Hii ni licha ya Manchester United kuendelea kujikokota tangu kuanza kwa kampeni mpya na kusajili ushindi mmoja pekee dhidi ya ‘The Seagulls’. (Goal).