NA ABOUD MAHMOUD

WASANII wa muziki wa taarab asilia visiwani Zanzibar wameshauriwa kuuendeleza muziki huo ambao umekuwa ukiitangaza nchi miaka mingi kitaifa na kimataifa na hivi sasa unaonekana kusahaulika.

Akizungumza na Zanzibar Leo, msanii mahiri wa muziki wa taarab Mohammed Issa Matona ,alisema kutokana na kuwepo kwa vikundi vya taarab ya kisasa, wasanii wengi hukimbilia huko, hali ambayo inatishia kusahaulika muziki huo kwa vizazi  vijavyo.

Alisema ni kweli hivi sasa muziki wa taarab umekuwa wa biashara lakini vyema wasanii pamoja na viongozi wakuu wa Serikali, wanaoshughulikia sanaa kuupigia chapuo ili uweze kuwa na hadhi kama iliyokuwepo hapo awali.

“Muziki wa taarab asili umeitangaza nchi yetu sana dunia nzima na wengi duniani wanajua huu ndio muziki unaoitambulisha nchi yetu, vikundi mbali mbali kama Culture na Ikhwan Safaa vimeweza kuzunguka dunia lakini leo muziki huu unasahauliwa, watu wameweka mbele biashara tukiendelea hivi,”alisema Matona.