BUJUMBURA, BURUNDI

Hali ya wasiwasi yatanda Burundi baada ya mbunge wa zamani wa upinzani kukamatwa, NCHINI Burundi, mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yamelaani kukamatwa na kufungwa jela kwa mbunge wa zamani wa upinzani, Fabien Banciryanino.

Banciryanino alikamatwa bila kibali chochote kutoka polisi au ofisi ya mashitaka na kisha kufungwa katika jela kuu ya Mpimba jijini Bujumbura wiki iliyopita, akishtumiwa kwa makossa ya uasi, kashfa dhidi ya kiongozi na kutaka kuhatarisha usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa mmoja wa wanasheria wake na kulingana na barua ambayo mbunge huyo wa zamani alituma kwa CNIDH, Tume Huru ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Burundi, aliulizwa maneno aliyotoa wakati wa kikao cha Bunge, mmwezi Februari 2020, alipokuwa bado mbunge.

Banciryanino alikuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa utawala wa katika bunge lililomaliza muda wake hivi karibuni.

Katika kikao hicho cha bunge cha Februari 2020, bunge la kitaifa lilipitisha muswada uliomuinua na kummpa cheo rais wa wakati huo Pierre Nkurunziza kuwa kiongozi mkuu wa uzalendo.

Katika mswaada huo, Banciryanino alikuwa mbunge pekee aliyetamka hadharani kupinga uamuzi huo, huku akielezea uhalifu mkubwa uliotekelezwa kwa miaka 15 ya utawala wa rais Pierre Nkurunziza.

Spika wa Bunge wakati huo Pascal Nyabenda alimtuhumu mbunge huyo na kusema kuwa madai aliyoyatoa bungeni hayana msingi.

Mbunge huyo wa zamani amekuwa akihofia usalama wake tangu muhula wake ulipomalizika miezi miwili iliyopita, ambapo siku 10 baada ya kukamatwa shirika la haki za binadamu ITEKA lilishutumu ukiukaji mkubwa wa katiba.