Leo hii wapenzi wasomaji wetu wa safu hii ya maakuli nimeamua kwa makusudi kuwatayarishia mlo ambao hautakuwa wa mafuta wala nazi kama tulivyozoea, kwa hakika ukipika leo hii basi uatatamani siku zote ufanye hivyo.

Mchemsho wa ndizi mbichi na samaki ni Chakula bora chenye virutubisho vyote vya kujenga mwili. Mchemsho kama huu ukila wakati wa mchana ni chakula bora kwa kujenga mwili wako na kuendelea kufanya kazi za kuendeleza maisha.

Basi ili uweze kufanikisha mlo huu ni lazima uhitaji vitu vifuatavyo.

MAHITAJI

Samaki 2

Ndizi (aina yeyote, katika mapishi haya nimetumia ndizi bukoba)

Keroti

Pilipili hoho

Vitunguu maji

Chumvi

Tungule

Ndimu

MAELEKEZO

Menya ndizi na uhifadhi kwenye chombo chenye maji ili zisipate kubadilika rangi.

Andaa samaki – osha, kata vipande vinavyofaa au kama unapenda mpike mzima – kamulia ndimu. Changanya samaki na limao. Kisha mhifadhi samaki pembeni.

Andaa tungule – osha na kisha menya tungule 3 na kuzikata vipande vidogo. Hifadhi kwenye chombo.

Menya vitunguu maji 2 vikubwa halafu kata kwenye vipande vidogo unavyopendelea.

Osha na kisha kata pilipili hoho 1 kubwa kwenye vipande vidogo. Fanya vivyo hivyo kwakeroti 1 kubwa

Weka ndizi kwenye sufuria au kikaangio kinachofaa kupikia

Weka vitunguu maji juu ya ndizi, halafu weka tungule juu yake, kisha malizia na karoti.

Weka samaki wako kwenye kikaangio kwa kuwapanga vizuri juu ya karoti.

Nyunyizia chumvi ya kutosha. Usiongeze mafuta maana kwenye samaki na vitunguu kuna mafuta ya kutosha, hivyo haina haja ya kuongeza zaidi.

Weka maji kiasi kama kikombe 1 kikubwa halafu funika na mfuniko usioruhusu mvuke kutoka. Hii inasaidia zile mboga mboga (karoti, pilipili hoho, kitunguu na tumgule) zichuje maji yake na kukipa chakula ladha na harufu nzuri.

Subiria kwa muda wa dakika 15 hadi 20 na mchemsho wako utakuwa tayari kuliwa.