RIYAD,SAUDIA ARABIA

HATICE Cengiz (Khadija Changiz), mchumba wa Jamal Khashoggi, mwandishi Msaudia aliyekuwa anaukosoa utawala wa kiimla wa nchi hiyo na ambaye aliuliwa kikatili na kinyama na maofisa wa Saudi Arabia ndani ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul Uturuki, amefungua rasmi mashitaka mahakamani dhidi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, asasi inayoitwa Taasisi ya Demokrasia kwa ajili ya Ulimwengu wa Kiarabu, iliteua mawakili wawili wa kumwakilisha Hatice Cengiz kufungua rasmi mashitaka dhidi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na maofisa wengine 20 waliohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi.

Kwa mujibu wa tangazo la taasisi hiyo, mashitaka hayo yameshakabidhiwa kwa mahakama ya kiidara ya Columbia mjini Washington, Marekani. 

Tarehe pili Oktoba 2018, Jamal Khashoggi mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, aliuliwa kikatili na kinyama na maofisa wa Saudia katika ubalozi wao mdogo mjini Istanbul Uturuki.

Maofisa hao walitumwa rasmi kutoka Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia kwenda kufanya mauaji hayo.

Baadhi ya wauaji hao waliwasili nchini Uturuki kwa ndege binafsi. Khashoggi muda wote alikuwa anaishi nje ya Saudi Arabia kwa kuhofia usalama wake kutokana na kuukosoa utawala wa bin Salman na baba yake.

Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilisema kuwa Muhammad bin Salman ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa Jamal Khashoggi.

Hata hivyo hivi karibuni mahakama moja ya kimaonyesho ilisikiliza kesi hiyo nchini Saudi Arabia na kuwatoa hatiani watuhumiwa wa mauaji hayo.

Siku ya Jumatatu ya tarehe 7 Septemba, Agnes Callamard, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya nje ya nchi alisema kuwa mchezo uliofanywa na mahakama hiyo ya Saudia ni kuzifanyia istihzai sheria na uadilifu.

Alisisitiza kuwa, mchakato wa kusikiliza kesi ya watuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi ulikosa uadilifu na uwazi.