Alitokea kambi za wakimbizi hadi mwanamitindo wa kimataifa

ZASPOTI

ADUT Akech aliezaliwa Disemba 25, 1999, ni mwanamitindo wa Sudani ya Kusini pamoja na Australia, ambae anafanya kazi na Umoja wa Mataifa kuunga mkono wakimbizi.
Akech alizaliwa Sudani ya kusini, na kukukulia Kakuma, Kenya, kwenye kambi kubwa ya wakimbizi, hadi umri wa miaka mitano.


“Kwa kweli sikuwa na vitu vingi, lakini nilikuwa na chakula na mahali pa kulala, sikuwa na nguo nyingi, lakini bado nilikuwa na kitu cha kuvaa” Alisema, kwenye mahojiano yake na jarida la Vogue, huko New York.


Ameamua kuifanya hadithi yake ya mafanikio kuwa mfano, kwamba anataka kusaidia watu kuelewa kwamba wakimbizi ni watu wa kawaida, kama watu wengine.
Alisema hataki kujulikana kama ‘Adut, mwanamitindo,’ bali anataka kujulikana kama mtu ambaye alifanya mambo mazuri, kwa kuhusika zaidi na misaada ambayo inabadilisha maisha ya watu.


Wakati akiwa na umri wa miaka 6 aliondoka Kenya pamoja na mamaake kuelekea Adelaide, Australia, ambako alikulia huko, alisoma na kuanza kazi yake ya mitindo akiwa na umri wa miaka 16.
Alianza kazi yake ya uanamitindo kwenye maonyesho ya mitindo ya mitaani, na baadae akaendelea kwa kufanya wiki ya mitindo ya mji maarufu wa Australia, Melbourne, ambapo alipata nafasi pia ya kushiriki katika Wiki ya Mitindo ya Paris.


Tangu aanze onyesho hilo la Saint Laurent kwenye Wiki ya Mitindo ya Paris, Akech amefanya maonyesho na kampeni kwenye kampuni za mitindo za kimataifa, miongoni mwao ni Chanel, Dior na Prada, pia kuonekana kwenye kurasa za mbele za majarida kama jarida la Vogue.


Mwanamitindo huyo, amewekwa katika Kalenda ya Pirelli ya 2018, iliyopigwa na mpiga picha mashuhuri ‘Tim Walker’, pamoja na Sasha Lane, pia alitakiwa kuwa balozi wa Wiki ya Mitindo ya Melbourne ya 2019.
Mwaka 2019, jarida la ‘Who’ liliandika Makala inayomuhusu Akech, lakini iliweka picha ya msichana mwengine mbali na yeye, alisema kosa hilo “halikutarajiwa na wala halisameheki”, hivyo jarida hilo lilimuomba msamaha.


Akizungumzia muonekano wa ngozi yake, Akech alisema tokea akiwa na umri mdogo, alikuwa akionewa kutikana na weusi wa ngozi yake, na jarida moja la Australia ilichafuliwa na malalamiko ya mfanyakazi kwamba sura yake haitavutia wasomaji wao.


“Itachukua muda kuona jambo hili linaleta mabadiliko lakini inanifanya nijivunie sana kuwa mimi ni mfano ambao ninaweza kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko hayo.” Alisema Akech.
Mnamo Disemba 2019, alichukua ushindi wa mwanamitindo wa mwaka ‘Model of the Year’ na alipewa tuzo hiyo katika hafla ya ‘British Fashion Awards’ huko London,


Takwimu za ‘models.com’, zinaonesha kuwa Akech kwa sasa yupo kwenye 50 bora ya wanamitindo.
Akech, mwenye umri wa miaka 19, alimuahidi mama yake atamaliza shule ya Sekondari, kuwa mfano bora na kumnunulia nyumba na gari na ameweza kutimiza ahadi zote.
“Hata nikiwa mwanamitindo tajiri zaidi ulimwenguni, bado nitakuwa mkimbizi, mimi ni mkimbizi,” adut.