NA ABOUD MAHMOUD

CHAMA cha ACT Wazalendo Jimbo la Kikwajuni kimesema endapo kitapata ridhaa ya kuchaguliwa wa wananchi wa jimbo hilo, kitahakikisha kinawekeza kwenye michezo ili kuibua vipaji vya watoto na kushiriki katika mashindano mbali mbali ya ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza na mwandishi wa Zanzibarleo, mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kikwajuni Dhamir Ramadhan Yakout,alisema kutokana na ilani yao kwa jimbo hilo imejipanga kuboresha maeneo ya michezo ili iweze kuendana na wakati .

Dhamir alisema mara baada ya kuchaguliwa na wananchi wa Kikwajuni atahakikisha anakifanyia matengenezo kiwanja cha mpira wa miguu cha Alabama na kuwa cha kisasa.

Alisema wataalamu wa ujenzi wamefanya makisio ya gharama za ujenzi wa kiwanja cha Kikwajuni kitafikia milioni 50,hivyo ofisi ya Mbunge na Mwakilishi itashirikiana na wadhamini kuhakikisha kiwanja hicho kinajengwa ndani ya miaka minne ya awamu ya kwanza ya uongozi wao.

“Tukipata ridhaa ya wana Kikwajuni ofisi ya Mbunge na Mwakilishi itachukua jukumu la kukifufua kiwanja cha mchezo wa mpira wa kikapu na kurudi katika hali ya ubora na pia kitawekewa majukwaa na kuanza kutumika katika mashindano yanayofanyika ndani ya nchi,”alisema.