Niko tayari kupokea matokeo yoyote

NA MWANTANGA AME

MGOMBEA wa Urais wa Chama cha ADA TADEA, amesema yuko tayari kukubali matokeo yatayojitokeza katika uchaguzi Mkuu utafianyika kuanzia kesho.

Katib aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo, Mjini Unguja, ambapo alisema aina yoyote ya matokeo yatayojitokeza atayapokea kwa vile katika ushindani kuna kushinda na kushindwa.

Alisema Chama chake kimejipanga kuona uchaguzi unafanyika kwa amani na hana wasi wasi wa kutumika mfumo wa kura ya mapema itayopigwa Oktoba 27 na ile ya 28, kwani mfumo huo alishiriki kuukubali kutumika kisheria ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Kutokana na hali hiyo, Khatib alisema atakuwa tayari kukubali matokeo yatayotolewa katika uchaguzi ujao kwa vile utafanyika kwa uhuru na wa haki kutokana na vyama kupewa nafasi ya kuweka wakala wao ndani ya vituo vya kupigia kura.

“Nitakuwa mnafiki nikihamasisha wanachama wangu waende wakapige kura tarehe ambayo haipo rasmi kwa wao kufanya hivyo wakati sheria inatungwa ilipelekwa Baraza la wawakilishi na mimi nikiwa mjumbe na nikaikubali kama nilikuwa sitaki hilo ningeliipinga huko sio kwa kuwalazimisha wananchi wangu” alisema Khatib.

Akiendelea alisema kiongozi yoyote anae hubiri siasa za chuki katika karne hii tayari ameonesha udhaifu wa kisiasa na sio vizuri kuliingiza taifa hili katika migogoro ambayo italisababisha nchi kuingia katika majanga.

“Viongozi wa kisiasa wasiwe na tamaa kulazimisha kuwa Rais wakati Mungu hajakuandikia usitoe kutoa kauli za vitisho mimi ninawaomba wananchi wasifuate maagizo yanayokwenda kinyume na sheria ya uchaguzi tuwakataze vijana wetu waume zetu na wake zetu tusikubali kubuzwa kisiasa” alisema.

Akiendelea alisema serikali ya Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, imejitahidi kufanya mabadiliko mbali mbali ya kimaendeleo ambayo yanahitajika kuendelezwa na sio kuvurugwa.