Mambo matano aliyotilia mkazo katika uhai wake

Na Mwandishi Wetu

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa April 13, 1922 katika kijiji cha Butiama, Mkoa wa Mara.  Aliongoza Tanganyika na baadae Tanzania kuanzia mwaka 1961 hadi 1985 alipoachia nafasi ya urais ambayo ilichukuliwa na Ali Hassan Mwinyi.

Baada ya kustaafu urais wa Tanzania kwa hiari yake, akiwa ameiongoza Tanzania kwa zaidi ya miaka 24, aliendelea kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) hadi mwaka 1990 alipong’atuka na kumwachia nafasi hiyo Ali Hassan Mwinyi.

Licha ya kustaafu urais na uenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere aliendelea kuitumikia Tanzania kama mshauri katika masuala mbali mbali, hasa pale alipoona mambo yanakwenda sivyo ndivyo. 

Alikuwa kiongozi aliyeipenda nchi yake kwa dhati na hakupenda kuona mambo yakienda shaghalabaghala.

Enzi za uhai wake, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitoa hotuba katika mikutano mbali mbali, ndani nan je ya nchi, ambazo alizitumia kusisitiza mambo mengi, kuanzia uchumi, siasa, dini na mengineyo yanayoihusu jamii.

Miongoni mwa mambo ambayo Mwalimu Nyerere alipenda kuyazungumzia ni pamoja na udini, ukabila, elimu, maradhi, umasikini,uongozi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (uliounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).

UKABILA:

Suala la ukabila ni jambo nyeti, ambalo Mwalimu Nyerere alipenda kuligusia katika hotuba zake nyingi alizozitoa katika matukio mbali mbali.

Mwalimu Nyerere alikemea ukabila kila alipopata nafasi ya kuzungumza na hakutaka kabisa kuwe na maswali kama vile wewe kabila gani?  Katika hilo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.  Sio kawaida kwa Watanzania wa sasa kuulizana kuhusu masuala ya ukabila.

“Niliwahi kukutana na mama mmoja pale New York (Marekani), anatokea Uganda.  Akaniambia kuwa aliwahi kufanyakazi katika Jumuia ya Afrika ya Mashariki … sisi watu wa Uganda tulikuwa tunajuana kwa makabila yetu; watu wa Kenya walikuwa pia wakijuana kwa makabila yao; huyu mkikuyu, huyu mluhya.  Lakini sisi Watanzania hatujui makabila ya watu. 

Nikamwambia mama ni wakati huo, sasa hivi Watanzania wanataka kujua makabila yao; ya nini kwani mnataka kutambika?  Majirani zetu walikuwa wanaiga kutoka Tanzania, sasa bila ya haya wala soni sisi tunataka kuulizana makabila?”  Aliwahi kuzungumza Mwalimu Nyerere,  katika Mkutano Mkuu wa CCM mwaka 1995.

DINI:

Dini ni jambo ambalo Mwalimu Nyerere alisisitiza sana katika hotuba zake, hasa kuwaasa viongozi wasitafute uongozi kwa kutumia dini.

“Mambo haya ya kuchochea chuki za dini yakianza na tukayapa nafasi, huwa hayana sumile, na ikifika wakati yakashika kasi hakuna wa kuzuia,” alisema Mwalimu Nyerere, katika moja ya mikutano aliyohutubia.

UJINGA:

Mwalimu Nyerere pia alikuwa akisisitiza sana juu ya masuala yanayohusu ujinga, umasikini na maradhi.  Alisema iwapo Tanganyika (wakati huo) na baadae Tanzania, itafanikiwa kuyamaliza mambo hayo, itakuwa miongoni mwa nchi itakayoendelea zaidi duniani.

“Nchi hii bado ni ya wakulima na wafanyakazi, hatuwezi kuwa nan chi ya watu wenye kudai na kudai.  Nawaomba ndugu zangu Watanzania, hatujalemaa sana, lakini kilema kipo.  Viongozi wetu wanadai na kudai tu, watu ni masikini, wachache hao wana nguvu ya kuongoza nchi hii, ndio wanadai tu,” aliwahi kutamka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

UONGOZI:

Katika suala la uongozi, maadili ya uongozi ni jambo ambalo Mwalimu Nyerere aliliweka mbele sana.  Alipenda kuona Tanzania inakuwa na viongozi wanaoweza kukidhi matarajio ya Watanzania.

“Watanzania wanataka mabadiliko.  Wasipoyapata ndani ya CCM watayapata nje ya CCM … Inatakiwa ukiulizwa swali kwamba huyu atapiga vita rushwa; jibu lake litoke ndani ya moyo.  Nchi yetu ni masikini, bado haijawa ya matajiri.  Hivyo tunataka tuendelee kushughulikia umasikini wetu na matatizo ya wananchi.  Tunataka nchi yetu ipate kiongozi safi,” aliwahi kutamka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika moja ya mikutano yake.

MUUNGANO:

Katika vitu ambavyo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa akitamani kufanya ni kuunganisha nchi za Afrika ya Mashariki na kuwa na uongozi wa pamoja, ingawa hakufanikiwa sana katika hilo.

 Alichofanikiwa ni kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964.

“Matumaini yangu ilikuwa ni kuunganisha nchi za Afrika ya Mashariki na kuwa muungano mmoja.  Kwa upande wa Zanzibar niliongea na Karume, akasema niko tayari waite watu wa magazeti sasa hivi.  Nikamwambia tufanye taratibu na tutafanikiwa.  Kwa nchi za Afrika ya Mashariki tungekuwa na serikali tatu za kila nchi na Serikali ya Muungano; yaani Tanganyika (Tanzania) na Muungano,” alisema Mwalimu Nyerere.

NUKUU ZA MWALIMU NYERERE:

Hakuna Taifa lenye haki ya kufanya maamuzi kwaajili ya taifa jengine; hakuna watu kwaajili ya watu wengine.

Watu wanapaswa kuhusishwa ili kufikia maendeleo ya kweli. Elimu sio njia ya kuepuka umasikini, ni njia ya kupigana nao.

Umoja hautatufanya kuwa tajiri, lakini unaweza kuwezesha kuiepusha Afrika na watu wa Afrika kutoheshimiwa na kudhalilishwa.

Katika Tanganyika tunaamini kwamba watu waovu ni watu wasiomuamini Mwenyezi Mungu, wanaoweza kufanya rangi ya mwili wa binaadamu kuwa kigezo cha kumpa haki zake za kiraia.

Demokrasia sio chupa ya Coca-Cola, ambayo unaweza kuiagiza.  Demokrasia inapaswa kuendelezwa kulingana na nchi yenyewe.

Hatuwezi kuwa na matumaini ya kutatua matatizo yetu kwa kujifanya kuwa hayapo.

Itakuwa yote ni makosa, na sio jambo la muhimu, kuhisi kuwa lazima tusubiri hadi viongozi wafe ndio tuanze kuwakosoa.