NAIROBI,KENYA

WATAKAOSABABISHA  machafuko wakati wa mchujo wa vyama vya siasa watawekwa gerezani kwa miaka mitano au kulipa faini ya Shilingi milioni kumi ikiwa mswaada mpya utatungwa.

Muswada wa Sheria ya Mashitaka ya vyama vya Kisiasa, 2020 unapendekeza adhabu kali kwa wale wanaosababisha vurugu au kutoa rushwa ili kushawishi matokeo ya kura.

Inaelezwa kwamba mtu yoyote ambaye anatumia au kutishia kutumia nguvu yoyote, vurugu au kutoa na  kupokea rushwa anatenda kosa la uchaguzi.

“Mtu kama huyo anatenda kosa na atawajibika kwa kosa la kulipa faini isiyozidi shilingi milioni kumi au kifungo kwa kipindi kisichozidi miaka mitano au adhabu zote mbili kwa pamoja,” unaeleza muswada huo.

Wahalifu pia ni pamoja na wale wanaotumia au kutishia kuumiza, au kupoteza mtu au dhidi ya mtu wakati wa mchujo wa chama ili kumshawishi au kumlazimisha mtu huyo kumuunga mkono mgombeaji fulani au kupiga kura kwa njia fulani au kuacha kupiga kura.

Kwa kuongezea, muswada huo unataka kukomesha tabia hiyo ambapo maofisa wa chama wanajiandikisha au kuandikisha wanachama kwa hiari yao, kuharibu rejista au kutotumia rejista ya uanachama wa chama wakati wa uchaguzi wa chama.

Viongozi hao watafungwa kwa mwaka mmoja au kutozwa faini ya Shilingi milioni tano ikiwa watapatikana na hatia ya kosa hilo.

“Mtu ambaye kwa makusudi na bila sababu ya haki anazuia au kumzuia mtu mwengine kupata kituo cha kupigia kura au kupiga kura katika kituo cha kupigia kura ambapo mtu huyo mwengine anastahili kupiga kura atatenda kosa na atawajibika kwa kosa la kulipa faini isiyozidi Shilingi  milioni moja au kifungo kwa kipindi kisichozidi miezi sita au zote mbili,”mswaada huo unasema.

Ikiidhinishwa na Bunge na kusainiwa kuwa sheria, muswada huo utamaliza machafuko ambayo mara nyingi yanatikisa vyama vya siasa kila mchujo wa uchaguzi.