NA ALI MASSOUD  KOMBO ,PEMBA

WANANCHI wa jimbo la Micheweni  wametakiwa  kuendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi ( CCM)  kuwa ndicho chenye  kuleta maendeleo  kwa jamii kwani  mafanikio  makubwa  yaliopatikata  katika maeneo mbali mbali

yameletwa na chama hicho.Kauli hiyo ime tolewa  Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM, Sofia Muhamed Mzirai , huko katika kijiji cha Kiuyu Mbuyuni Micheweni, wakati alipokuwa akiwanadi wagombea wa Ubunge ,Uwakilishi  na Madiwani wa jimbo la Micheweni.

Alisema kuwa  mafanikio makubwa yamepatikana  kwa kila kijiji  hivyowaendee kukiamini chama, kwani ndicho chama  chenye kujua  matatizo ambayo yamekuwa yakiwakwaza Wananchi  na kuyatatuwa kwa wakati.

“Chama chetu cha  CCM, kimeleta mambo mengi katika vijiji mbali mbali katika nchi ya Zanzibar  kimeboresha umeme, maji, huduma za afya  na kusaidia kupunguza usumbufu ulio kuwa ukiwapata wanawake wengi katika maeneo mbali mbali  ikiwemo Kiuyu Mbuyuni” alisema Sofia.

Naye Asia Sharifu Omar,  ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa mkoa wa Kaskazini Pemba,  aliwataka vijana kuacha kutumika vibaya katika kuashiria kuvuruga amani na utulivu uliopo. Alieleza kuwa vijana wengi wamekuwa wakitumiwa  vibaya  na wana siasa kwa lengo la kuvuruga amani  na kuwataka vijana kuwa makini na wanasiasa ambao hawapendi wananchi kuona wametulia.

“Jamani vijana  mjitenge na wanasiasa  wasio penda amani kwani sio watu wazuri hawawatakii  mema  kwani wao huwa hawajihusishi katika vurugu na kuwaachia nyinyi vijana  hivyo atakae kuja kwa kuwahamasisha kufanya vurugu mkataeni sio kiongozi bora huyo” alisema Asia.