NA LAYLAT KHALFAN

MKUU wa Wilaya ya Kusini Unguja, Idrissa Kitwana Mustafa, amesema suala la uwekezaji na utalii bado limekua likiwatesa wananchi ndani ya wilaya hiyo kwa kuwafukuza kazi kiholela bila ya kuwepo utaratibu maalum.

“Tabia ya kuachisha wafanyakazi kazi na kuwafungisha mikataba wengine bila ya kumaliza mikataba yao si utaratibu mzuri nitahakikisha napambana nalo hadi nijue mwisho wake kwani huu unaofanyika ni unyanyasaji”, alisema.

Kitwana Alifahamisha kuwa, katika kupambana nalo hilo hivi sasa wameanza kupita mahotelini kwa kuangalia mikataba ya wafanyakazi, ili kuona namna gani mfanyakazi anaendelea kufanyakazi.

“Yapo mikataba ambayo anamiliki mwenyewe mwekezaji wakati mfanyakazi anashindwa kuwa na hata kopi, ili ikitokezea tatizo ajue wapi pakupata haki zake anazostahiki”, alisema.

Alisema mara nyingi wanakua wakiwashtaki wawekezaji kwa kuwapeleka kwa wanasheria wao, lakini hali inaonekana bado kuendelea kushamiri siku hadi siku.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Khamis Mwinyi Mohamed, aliwataka waajiri hususan katika sekta binafsi kuhakikisha wanafuata sheria za kazi katika kuajiri na kuwaondoa wafanyakazi kazini.