WAMAREKANI watashuka vituoni Novemba 3 mwaka huu kwa ajili kumchagua rais mpya atakayeliongoza taifa hilo kwa miaka minne ijayo kuanzia siku ya kwanza atakayoingia ikulu ya White House, Januari 20 mwaka 2021.

Uchaguzi wa Marekani mwaka huu umekuwa wa heka heke kubwa kutokana na taifa hilo kukabiliwa na mambo mbalimbali yakiwemo ya kisiasa, kijamii na hata suala la sera ya mambo ya nje ya nchi hiyo.

Kama kawaida mchuano mkali unaonekaba baina ya Donald Trump rais anayetetea kiti chake kutoka chama cha republican pamoja na Joe Biden makamu wa rais wa zamani wa taifa hilo akitokea katika chama democratic.

Hivi karibuni viongozi hao walichuana kwenye mdahali uliorushwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari ambapo ilikuwa fursa ya kupimwa na wapiga kura wa Marekani.

Hata hivyo, mdahalo wao inasemekana ni miongoni mwa mdahalo mbaya kuwahi kutokea katika histoaria ya taifa hilo kwani walishindwa kujibu hoja zilizotarajiwa kuwashibisha wapiga kura ili wafanye maamuzi na badala yake ulikuwa madahalo wa vita vya maneno.

Baada ya mdahalo wa Trump na Biden kumalizika wiki moja iliyofuata ulifanyika madahalo uliowahusisha wagombea wenza wa viongozi hao ambapo atakayeshinda mmoja wapo atakuwa makamu wa rais wa taifa hilo.

Huu ulikuwa mdahalo uliowakutanisha na kuwatoa kijasho Mike Pence mgombea mwenza na makamu wa rais wa sasa wa Marekani na mgombea mwenza wa chama cha democratic, seneta Kamala Harris.

Madahalo baina ya Pence na Kamala kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Marekani wanaeleza kuwa nao hawajazungumzia jambo lolote jipya na kwamba mara nyingi wagombea wenza hao hawakujibu baadhi ya masuala walioulizwa na mwendesha mdahalo Susan Page.

Hata hivyo, suala la jinsi utawala wa sasa wa rais Donald Trump ulivyokabiliana na janga la mripuko wa ugonjwa wa corona lilichukuwa nafasi ya juu, katika wakati ambapo rais huyo na baadhi ya washauri wake wakiwa wamepata maambukizi na wanaugua ugonjwa huo.

Kulingana na utafiti wa maoni wa vyombo mbali mbali ni kwamba wamarekani wamegawika karibu sawa kwenye mdahalo baina ya Pence na Kamapa juu ya nani ameweza kutetea vilivyo ajenda katika mdahalo wao huo wa kwanza na wa pekee.

Alipoanza kuchukua nafasi kwenye mdahalo huo, Kamala alisema Trump ameshindwa kukabiliana na janga la maradhi ya corona kiasi kwamba ugonjwa huo umekuwa janga kwa wananchi wa taifa hilo.

Kamala alisema, “Wamarekani wameshuhudia kile ambacho ni kushindwa vibaya sana kufanya kazi kukabiliana na janga la ugonjwa wa corona kwa utawala ulioko madarakani katika historia ya nchi yetu”.

Kwa upande wake Pence alimjibu seneta huyo kwa kueleza kuwa, “haikuwa hivyo, rais Trump alisitisha safari kutoka China kuliko kuwa kitovu cha virusi hivyo, akipunguza kasi za kusambaa kwa ugonjwa mwishoni mwa mwezi Januari”, alisema.

Akifafanua hoja hiyo, Pence alisema, “Kwa mara nyingine tena Wamarekani wanahaki kufahamu kwamba Joe Biden alipinga uamuzi wa rais Trump kusitisha safari zote kutoka China”.

Zaidi ya hayo Pence na Harris walizungumzia juu ya namna utawala wa Trump ulivyokabiliana na uchumi, sera za kigeni, mabadiliko ya hali ya hewa, ukosefu wa ajira na vita vya biashara baina ya nchi hiyo na China.

Kamala aliongeza kwa kusema “kwa sababu ya hicho kinachojulikana kama vita vya biashara na China, Marekani imepoteza nafasi 300,000 za ajira katika viwanda”.

Naye Pence kwa mara nyingine akipinga jambo hilo akisema, “Tumepoteza vita vya biashara na China? Joe Biden hajapata kamwe kupigania vita hivyo. Biden amekua mtetezi wa China ya kikomunisti mnamo miongo kadhaa sasa”.

Suala tete kwenye mdahalo lilikuwa ni mvutano kati ya Warepublican na Wademokrat juu ya kuteuliwa kwa jaji mconservative kuchukuwa nafasi katika mahakama ya juu iliyoachwa na hayati jaji Ruth Bader Ginsburg aliyefariki mwezi Septemba mwaka 2020.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kazi kubwa ya wagombea kiti cha makamu wa rais katika mdahalo ni kuepusha kufanya makosa yatakayo umiza misimamo ya wagombea wenza wao.

Kwa upande wake Prof. Anra Gillespie kutoka chuo kikuu cha Emory anasema wagombea hao waliweza kutetea sera zao vizuri.

Prof. Gillespie alisema, “Ninadhani kwa sehemu kubwa walifanikiwa kutodhuru kampeni zao. Hivi sasa makamu wa rais Pence yuko katika hali tofauti kwa sababu yeye ni sehemu ya serikali inayotetea madaraka yake na hivyo ni lazima ajibu kasoro na mafakinio ya utawala wa Trump”, alisema.

Naye Rich Meagher kutoka chuo kikuu cha Randolph-Macon alisema mdahalo huu ulikuwa na umuhimu mkubwa katika uchaguzi, ambapo karibu watu milioni nne wameshapiga kura zao katika majimbo yanayoruhusu upigaji kura mapema.

Meagher alisema, “watu hawampigi kura makamu rais, wanawapigia kura rais. Lakini mwaka 2020 mambo ni tofauti. Tuna wagombea wawili wazee kuliko wakati mwengine wowote ule. Tuna mgombea mmoja anaetetea kiti chake ambaye anaugua ugonjwa mmoja wa hatari”.

Na hivyo wagombea hao wa nafasi ya makamu wa rais wanalazimika kuwa tayari kuchukua nafasi ya rais ikiwa rais atafariki akiwa madarakani au hawezi kufanya kazi zake.

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni hadi Oktoba 10 mwkaa huu Joe Biden anaongoza kwa wastani asilimia 10 dhidi ya Trump na yuko katika nafasi nzuri kwenye majimbo yenye ushindani mkubwa.

Inaripotiwa kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya Marekani idadi kubwa kabisa ya wapiga kura wametumia njia ya posta kupiga kura zao na tayari mamilioni wameshapeleka kura zao posta.