NA TATU MAKAME

Waziri wa Kilimo,Maliasili, Mifungo na Uvuvi Zanzibar, Mmanga Mjengo Mjawiri  amesema ipo haja ya kuongeza bidii katika ufugaji wa asali kwa wananchi, ili kuongeza upatikanaji wa zao hilo hapa nchini.

Mjawiri alisema hayo Maruhubi Mkoa wa Mjini Magharibi wakati alipozungumza na watendaji wa Wizara hiyo pamoja na wadau wanaohusika na masuala ya uhifadhi wa mazingira katika Msitu wa hifadhi ya Taifa uliyopo Jozani Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisisitiza wananchi kujishirikisha na ufugaji wa nyuki kwani wanaweza kujikwamua na hali ya umaskini pale watakapozalisha asali kwa wingi kwani bado mdogo ingawa soko lake kubwa kwa matumizi ya zao hilo.

“Kwa mwaka huu tulizalisha tani 13.5 na kwenye ilani Wizara ilitakiwa izalishe tani 15, bado ipo haja ya kuongeza uzalishaji”,alisema Mjawiri.

Aliwataka wadau kuwasisitiza wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu kwa lengo la kuongeza ufugaji wa asali na njia hiyo itapunguza uharibifu wa mazingira.

Naibu Katibu Jumuiya ya uhifadhi wa mazingira Jozani (JECA)

Awesu Shaabani Ramadhani, alisema bado wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi misitu kwa manufaa vizazi vya sasa na baadae.