NA LAYLAT KHALFAN

MWENYEKITI mstaafu wa CCM mkoa mjini Kichama, Borafya Ame Silima, amewatahadharisha wanachama wa Chama cha Mapinduzi kutothubutu kwenda kupiga kura Oktoba 27 kwa ajili ya usalama wao.

Alisema siku hiyo itakuwa na watu maalum ambao wanahitajika kupiga kura na kwa sababu maalum, hivyo wanachama hao ni vyema kwenda kupiga kura Oktoba 28 kwa kuitilia CCM ili iendelee kubaki madarakani.

Borafya, alitoa tahadhari hiyo, katika ufungaji wa kampeni za kuwanadi wagombea wa chama hicho kwa jimbo la Amani wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.

Alisema kura ni muhimu na ni msingi wa nchi, hivyo hakuna sababu ya kufanya mzaha katika kufanikisha suala hilo.

Alifahamisha kuwa, jukumu lao kubwa na la kihistoria ni kuimarisha umoja na kuleta mapinduzi ya ujamaa Tanzania na kuendeleza mapambano ya uongozi kwa Afrika na duniani kote.

“Lazima kuwe na chombo madhubuti kwa uongozi kitakachounganisha wakulima, wakwezi na wafanyakazi ili kuwafanya watu wote kuwa wamoja”, alisema.

Alisema walikuwa wanyonge na kunyonywa na mabepari, hivyo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekuwa mstari wa mbele kuendeleza mapinduzi hayo huku ikiamini kuwa binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshma na utu wake bila ya kunyanyasika.

Naye Mwenyekiti wa CCM jimbo la Amani, Jastus Issac, alisema amani ni tunu ya taifa bila ya amani kamwe hawawezi kufanya jambo lolote litakaloweza kuiletea nchi  maendeleo.

Kada wa CCM, Baraka Shamte, aliwatahadharisha wananchi kuwakataa viongozi wanaochochea vurugu kwani wanaweza kuwasababishia matatizo makubwa.

Mapema Mbunge wa Afrika mashariki, France Haji Nkui, alisema lazima viongozi wa jimbo wawe na uzoefu wa kutambua changamoto ndani ya majimbo yao ili waweze kuwatatulia wananchi kero zao ambazo zinawakabili.

 Mgombea Ubunge jimbo  hilo, Mussa Hassan Mussa, alisema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuendelea kuongoza tena jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano atahakikisha anawapatia elimu vijana itakayowawesha kunyanyua vipaji vyao kwa lengo la kujikimu kimaisha.

Mapema Mgombea Uwakilishi wa jimbo hilo, Rukia Omar Ramadhan Mapuri, alisema endapo atapata ridhaa ya wananchi atawasimamia wanawake katika vikundi vyao na wenye mahitaji maalum kwa kuwawezesha ili kujikomboa na umaskini.