NA MAULID YUSSUF, WEMA

WANAFUNZI wa kidato cha nne Mkoa wa Kusini Unguja, wametakiwa kushughulikia zaidi masomo yao, ili kuweza kufaulu vizuri katika mitihani yao inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao.  
Ofisa wa Elimu Mkoa wa  Kusini Unguja, Mwalimu Mohammed Haji Ramadhan, amesema hayo wakati akizungumza na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Makunduchi na Ukongoroni walipofanya ziara katika Mkoa wa Kusini Unguja, Alisema Mkoa huo, umeonekana kila mwaka kuwa karibu na mwisho katika matokeo ya mitihani, hivyo  amewataka kubadilisha mitazamo hiyo kwa kuleta ufaulu mzuri mwaka huu.
Aidha aliwataka Walimu wa Mkoa huo, kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwaonesha mbinu mbali mbali, ambazo zitawasaidia wanafunzi wao kuhakikisha wanafanya vizuri katika mitihani yao na kuweza kufaulu daraja la kwanza.    
Aliwataka kila mwalimu kuhakikisha wanajipangia mpango wake mwenyewe na kujitathmini, ili kufikia malengo hayo.  
Nae Ofisa Elimu Sekondari, Mwalim Mussa Abduraby, amewataka walimu kutenga muda wa kuzungumza na wazazi pamoja na wanafunzi juu ya suala la elimu, ili kuhakikisha Mkoa huo unapasisha vizuri.
Nae Ofisa huduma za wanafunzi kutoka Idara ya elimu Sekondari WEMA, Rukia Jabir, amewataka wanafunzi kuacha kujishughulisha na mapenzi, kwani bado wakati wao haujafika na badala yake washughulikie masomo yao, ili kujitengenezea mustakbali mzuri wa maisha yao ya baadae.