NA ABOUD MAHMOUD

MABINGWA wa soka ligi kuu ya Zanzibar, Mlandege FC inatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi ya wiki  hii, kuvaana na wekundi wa Msimbazi Simba SC, katika mechi ya kirafiki kwenye uwanja wa Chamanzi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Zanzibar Leo kocha mkuu wa klabu hiyo, Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ alisema mechi hiyo iliyopangwa kuanza majira ya saa 11:00 za jioni itasaidia kufika malengo waliyoyakusudia.

Kocha huyo alisema lengo la kucheza mechi hiyo ni kuwapa uzoefu wachezaji wake ili kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

“Tunatarajia kucheza na ndugu zetu wa Simba, naamini mechi hii itatusaidia kujua makosa yetu, ili tufanye vyema katika mashindano tunayotarajia kwenda kushiriki pamoja na kujua mbinu mbali mbali za michezo ya kimataifa,”alisema Kiduu.